Na Mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
ONGEZEKO kubwa la bei za mafuta nchini limeiweka sekta ya ujenzi katika wakati mgumu, huku likihatarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuongeza gharama za ujenzi,huku Wakandarasi wazawa wakadai kupitia magumu kwenye mikataba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA), Samuel Marwa, alisema ongezeko hilo si mabadiliko ya kawaida ya soko bali ni mshtuko mkubwa wa kiuchumi unaotokana na sababu za nje.
Marwa alitoa kauli hiyo hapo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwasilisha taarifa ya pamoja ya TUCASA, Chama cha Wakandarasi Tanzania (CATA) na Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania (TWCA), kuhusu athari za kupanda kwa bei za mafuta katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini.
Alisema takwimu za EWURA pamoja na tathmini ya Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) zinaonyesha kuwa kati ya Januari na Mei 2026 bei ya dizeli iliongezeka kwa takribani asilimia 55.8, huku petroli ikipanda kwa asilimia 48.1.
Alisema ongezeko hilo limeongeza gharama katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ikiwemo uendeshaji wa mitambo, uchimbaji wa malighafi, uzalishaji wa lami na zege, pamoja na usafirishaji wa vifaa vya ujenzi.
Kutokana na hali hiyo, wakandarasi wameanza kukabiliwa na kupanda kwa gharama za pembejeo za ujenzi, upungufu wa mtiririko wa fedha, ongezeko la gharama za mikopo, ucheleweshaji wa miradi na hatari ya migogoro ya kimkataba.
Marwa alisema changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kutokana na ucheleweshaji wa uthibitishaji na malipo ya kazi zilizokamilika katika baadhi ya miradi ya umma, jambo linalowalazimu wakandarasi kuendelea kutumia fedha zao au kukopa ili kulipa wafanyakazi, wasambazaji wa vifaa, wakandarasi wadogo na taasisi za fedha.
Alisisitiza kuwa athari za hali hiyo haziwahusu wakandarasi pekee, bali zinaweza kuathiri kasi ya maendeleo ya miundombinu ya taifa, ajira za wananchi, ushiriki wa wakandarasi wazawa katika uchumi pamoja na mfumo mzima wa ugavi unaotegemea sekta ya ujenzi.
Akizungumzia mapendekezo, Marwa amesema vyama hivyo vinaiomba Serikali kutambua rasmi ongezeko la sasa la bei za mafuta kama mshtuko wa kipekee wa kiuchumi unaoathiri mikataba ya miundombinu inayoendelea, na kuweka mwongozo wa pamoja utakaosaidia taasisi za umma kushughulikia athari hizo kwa usawa.
Pia walipendekeza kuruhusu kwa muda wakandarasi waliopo kwenye mikataba ya bei zisizobadilika kuwasilisha madai yanayoweza kuthibitishwa yaliyotokana na ongezeko la gharama za mafuta, pamoja na kuharakisha uthibitishaji na malipo ya madai halali ya wakandarasi ili kurejesha mtiririko mzuri wa fedha katika sekta hiyo.
Aidha, vyama hivyo vinataka maboresho ya muda mrefu katika mfumo wa manunuzi ya umma, ikiwemo kufanya mapitio ya mikataba sanifu ya PPRA ili kujumuisha masharti ya kukabiliana na mishtuko mikubwa ya kiuchumi, kuweka utaratibu wa marekebisho ya bei pale gharama zinapopanda kwa kiwango kikubwa na kuimarisha uimara wa mfumo wa manunuzi dhidi ya misukosuko ya baadaye.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment