Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unapenda kuujulisha umma kuwa watetezi wa haki za binadamu wawili, Jackson Martine Kabalo na Joseph Chaviruka Mrindoko, maarufu kama “Wachokonozi”, wameachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Arumeru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuendelea na ushahidi katika Shauri la Jinai Na. 000017735/2025.
Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa tarehe 26, 27 na 28 Mei 2026 pamoja na tarehe 4 na 5 Juni 2026. Katika tarehe hizo, upande wa Jamhuri uliwasilisha shahidi mmoja pekee mnamo tarehe 26 Mei 2026 ambaye alikuwa shahidi wa saba (7). Hata hivyo, katika tarehe zilizofuata upande wa mashtaka haukuwa na mashahidi wala kutoa sababu za msingi za kutokuwepo kwao.
Mahakama ilieleza kuwa tayari ilikuwa imetoa maelekezo kutokana na shauri hilo kuchukua muda mrefu na kwa kuzingatia umuhimu wa kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati bila ucheleweshaji usio wa lazima. Kutokana na kushindwa kwa upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi, Mahakama iliamuru washitakiwa waachiwe huru chini ya Kifungu cha 242(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Marejeo ya Mwaka 2023.
Ikumbukwe kuwa shauri hili lilianzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kama Shauri la Jinai Na. 15727/2025 ambapo tarehe 27 Julai 2025 upande wa Jamhuri uliomba kuondolewa kwa shauri hilo kwakuwa haukuwa tayari kuendelea nalo (nolle prosequi), na Mahakama ikaamuru washitakiwa waachiwe huru. Hata hivyo, siku hiyo hiyo walikamatwa tena na kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru kwa mashtaka yale yale bila maelezo ya msingi kutolewa kuhusu hatua hiyo.
Mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ni mawili ambayo ni: Kutoa taarifa za uongo mtandaoni; na Kufanya shughuli za utoaji wa maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni.
Katika kipindi chote cha mwenendo wa shauri hili, washitakiwa walikuwa wanatetewa na mawakili kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao ni Wakili Simon Mbwambo na Wakili Ally Mhyellah wa mkoani Arusha.
THRDC inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa haki za msingi, ikiwemo haki ya kusikilizwa kwa wakati, haki ya kupata dhamana pale inapowezekana, pamoja na
matumizi sahihi ya mifumo ya sheria bila kuathiri uhuru wa kujieleza na haki nyingine za kikatiba.
Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Juni 06, 2026

No comments:
Post a Comment