Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba, amesema Serikali haina mzaha kuhusu ulinzi wa Watanzania na rasilimali za nchi, akifafanua masuala hayo hayana upande.
Dkt. Mwigulu amesema mwaka jana mwishoni kulitokea mambo yaliyoumiza Watanzania, akisema hataki kuona Taifa likipitia au kurudia kilichojiri katika mwaka huo.
Akizungumza na wananchi wa Ikungi mkoani Singida, leo Jumamosi Juni 27,2026, Dkt. Mwigulu amesisitiza usalama wa nchi, hauna makundi, akisema licha Tanzania kuwa na vyama vya siasa, lakini vipo kwa sababu kuna Taifa.
“Tunaweza kufanya ibada kama kuna amani, pakichafuka waulizeni, hivyo kunapokuwa na viasharia vya kukosekana kwa usalama wa nchi, kipaumbele chetu ni kulishughulikia jambo hilo,” amesema Dkt Mwigulu.
Amesema Serikali haina ugomvi na vyama vya siasa, akisema hata yeye ametokana na chama cha siasa, lakini lazima wahakikishe Watanzania na Taifa kunakuwa na usalama.
“Hatupuuzi hilo ni jambo la kipaumbele, hatupuuzi hata chembechembe linapokuja jambo la nchi na usalama wa wananchi,” amesema Dkt Mwigulu.
Amesema Seriakali imefuatilia na kujiridhisha kuwa kuna watu wasiotakia mema Tanzania wanafanya michezo ya kuwataka kuwatumia vijana wa Kitanzania kwa masilahi binafsi.
“Kama Serikali inawajibu wa kulinda nchi, maisha ya Watanzania na rasilimali hatuwezi kupuuza jambo la aina hiyo,” amesisitiza.

No comments:
Post a Comment