Na Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema kuwa sekta ya kilimo ndiyo msingi wa maisha na lishe ya wananchi, hivyo inapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi.
Akifungua Maonesho ya Kilimo Biashara yaliyofanyika katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Selian mkoani Arusha, Makalla alisema maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, watafiti, wadau wa maendeleo na wakulima.
Alisema mafanikio ya kilimo biashara yanategemea uwezo wa wakulima kukubali na kutumia teknolojia mpya zinazoongeza tija na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Makalla alieleza kuwa wakulima watakaoendelea kutegemea mbinu za zamani za kilimo wataathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kujitokeza.
Alisisitiza kuwa wakati umefika wa kuachana na kilimo cha jadi ambacho kwa kiasi kikubwa kimepitwa na wakati na badala yake kutumia teknolojia za kisasa.
Aidha, aliwataka wakulima kuongeza thamani ya mazao yao ili kupata masoko yenye ushindani na kuongeza kipato.
Makalla alisema ni muhimu kwa wakulima kulichukulia kilimo kama biashara badala ya shughuli ya kujikimu pekee.
Aliongeza kuwa sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika usalama wa taifa kutokana na nafasi yake katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na malighafi za viwandani.
Pia aliwahimiza wakulima kuendelea kutumia mbegu bora pamoja na teknolojia mbalimbali zinazotokana na tafiti za kisayansi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhimishaji Teknolojia kutoka TARI, Dkt. Sophia Kasehenge, alisema Tanzania inapaswa kuongeza uzalishaji wa chakula ili kukidhi ongezeko la idadi ya watu.
Alisema kiwango cha ongezeko la watu nchini Tanzania ni asilimia 3.1, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 0.9 duniani na asilimia 2.5 barani Afrika, hali inayoongeza mahitaji ya chakula.
Dkt. Kasehenge aliwataka wakulima kutumia teknolojia za kisasa pamoja na huduma za wataalamu wa utafiti kutoka vituo vya TARI vilivyopo nchini.
Naye Mkurugenzi wa TARI Selian, Dkt. Caresma Chuwa, alisema kaulimbiu ya maonesho hayo inalenga kuwahamasisha wakulima kutumia teknolojia na huduma zinazotolewa na kituo hicho ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Dkt. Chuwa alisema TARI inaendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kutoa suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo nchini.
Alibainisha kuwa matokeo ya tafiti hizo yameendelea kuleta mabadiliko chanya katika uzalishaji wa mazao na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria maonesho hayo walisema yamekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha uzalishaji wao, wakieleza kuwa baada ya kushiriki maonesho ya mwaka jana wengi wao walibadili aina ya mbegu walizokuwa wakitumia na kupata mavuno bora zaidi.
Maonesho hayo yamewakutanisha watafiti, wakulima, wasindikaji wa mazao, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa kilimo kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuongeza tija na kukuza kilimo biashara nchini.



No comments:
Post a Comment