CPA Makala aipa shavu ITRACOM Kwa uzalishaji wa mbolea bora - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 11 July 2026

CPA Makala aipa shavu ITRACOM Kwa uzalishaji wa mbolea bora

 




Na Mwandishi wetu, Arusha 


maipacarusha20@gmail.com 


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amosi Makala, ameipongeza kampuni ya uzalishaji wa mbolea ya Itracom yenye makao makuu Nala, mkoani Dodoma, kwa mafanikio yake ya kuzalisha aina 14 za mbolea zinazolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.


CPA Makala alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya Kilimo Biashara yanayoendelea katika viwanja vya TARI Selian, jijini Arusha, ambapo alipata fursa ya kujionea bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.


Alisema uwekezaji unaofanywa na Itracom una mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuwapatia wakulima mbolea zenye ubora zinazosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao.


Aidha, aliitaka kampuni hiyo kuendelea kufanya tafiti zaidi ili kubuni aina mpya za mbolea zitakazokidhi mahitaji ya wakulima katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.


CPA Makala alisema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya pembejeo bora, hivyo kampuni kama Itracom zina nafasi kubwa ya kusaidia kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini.


Pia aliwahimiza wakulima kutumia mbolea zinazozalishwa na kampuni hiyo, akisema zimeendelea kufanya vizuri sokoni na zimeonyesha matokeo chanya katika uzalishaji wa mazao.


Kwa upande wake, Meneja wa Agronomia na Utafiti wa Kampuni ya Itracom, Dkt. Tulole Lugendo, alisema kampuni hiyo inazalisha aina 14 za mbolea zilizofanyiwa tafiti na kuthibitishwa kuwa na ufanisi mkubwa katika uzalishaji wa mazao.

Alisema dunia kwa sasa inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo matumizi ya mbolea bora ni muhimu ili kuwasaidia wakulima kupata mavuno mengi na yenye ubora.


Dkt. Lugendo alibainisha kuwa miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ni mbolea ya FOMI, ambayo imeendelea kupata matokeo mazuri katika mashamba ya wakulima.


Aliongeza kuwa kampuni hiyo inashirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za utafiti ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea zinazokidhi mahitaji ya mazao na aina tofauti za udongo.


Aidha, alisema Itracom hutumia muda mwingi kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea pamoja na namna ya kutambua afya ya udongo, huku akiwahimiza kutumia mbolea ya FOMI ili kuongeza tija na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

No comments: