NA SEIF TAKAZA – IRAMBA
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Alhaj Suleiman Yusuph Mwenda amezindua magari manne (4) ya kubebea wagonjwa na kutoa onyo magari hayo yasitumike bila utaratibu uliokusudiwa.
Alhaj Mwenda amesema anamshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Lameck Nchemba kukubali ombi la waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya hiyo alipokuwa na ziara katika Wilayani hiyo hivi karibuni.
“Magari haya ninayoyazindua leo hii yatumike kwa lengo lililo kusudiwa yasitumike kubebea
maiti na wakati wote yawe na mafuta, isiwe mgonjwa amezidiwa ili apelekwe hospitali
ikaonekana gari halina mafuta, nikigundua au kupata malalamiko kutoka kwa wananchi yeyote atakayehusika atupishe maana ameshindwa kuhudumia wananchi, madereva wawe makini kwani gari la kubebea wagonjwa huwa halifuati sheria za usalama barabarani kwani gari hizo ni za dharura” Alisisitiza - Alhaji Mwenda
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Afya ustawi wa jamii na Lishe Dkt Peter Luhega Janga
wakati akitoa taarifa ya magari ya kubebea wagonjwa alisema magari hayo ya kubebea
wagonjwa yanakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya bilioni moja pamoja na vifaa tiba vya
kutolea huduma za dharura vilivyopo kwenye magari hayo.
Dkt Janga amesema lengo la magari hayo ni kuokoa maisha ya wananchi wakati wa dharura,
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kuboresha mfumo wa rufaa za wagonjwa, kupunguza
gharama na changamoto za wagonjwa, kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati.
Amesema magari hayo ya kubebea wagonjwa ni kwa ajli ya vituo vya afya Ndago, Shelui,
Kinampanda na Tyegelo.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Innocent Msengi ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassani kwa kuboresha huduma za afya mchini, pamoja na shukurani za pekee kwa Waziri mkuu Dkt Mwigulu Lameck Nchemba
“Naungana na Mkuu wa Wilaya Alhaji Mwenda ni marufuku kwa gari la kubebea wagonjwa
kusafirisha maiti na kutumika katika kazi zingine za kiutawala, endapo itatokea watumishi
waliopewa dhamana ya kutumia vibaya nagari hayo achukuliwe hatua kali za kiutumishi” Alisisitiza Mwenyekiti huyo.
MWISHO

No comments:
Post a Comment