MOROGORO KUPAMBANA NA WADUDU WA KOROSHO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 14 July 2026

MOROGORO KUPAMBANA NA WADUDU WA KOROSHO

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com 


MAAFISA kilimo mkoani Morogoro wametakiwa kufikisha elimu ya kilimo bora cha korosho kwa wakulima wa vijijini ili kudhibiti wadudu na magonjwa ya zao hilo, hatua itakayoongeza uzalishaji na kusaidia serikali kufikia lengo la kuzalisha tani milioni moja za korosho.


Hayo yamesemwa na mkufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Mtwara, Joseph Mkude, katika shamba la korosho mkoani Morogoro, ambapo amewahimiza maafisa kilimo kuwafikishia wakulima elimu ya kudhibiti wadudu na magonjwa ya korosho kwa kuzingatia kanuni zote za kilimo bora ili kuepusha upotevu wa hadi asilimia 70 ya mavuno.


Amesema magonjwa na wadudu wa korosho yamekuwa yakisababisha hasara kubwa kwa wakulima kila mwaka, hivyo elimu ya mara kwa mara na ufuatiliaji wa mashamba ni njia muhimu ya kuongeza tija na ubora wa zao hilo.


Kwa upande wake, mtafiti kutoka TARI, George Lucas, amesema matumizi ya mbegu bora, ufuatiliaji wa mashamba na usimamizi sahihi wa magonjwa ni muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji wa korosho.


Ameongeza kuwa tafiti zinaendelea kufanyika ili kubaini mbinu bora zaidi za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye zao la korosho kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la wadudu waharibifu.

Mwakilishi bodi ya pamba

Naye Afisa Kilimo kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, Tawi la Morogoro, Edson Mbande, amewataka maafisa kilimo kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wakulima wote ili kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa korosho.


Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Kaizer Kaluwa, amesema wakulima wanapaswa kuandaa mashamba yao vizuri na kutumia viuatilifu vinavyopendekezwa kwa wakati ili kudhibiti wadudu na magonjwa ya korosho.


Amesema ushirikiano kati ya maafisa kilimo, taasisi za utafiti na wakulima utasaidia kuhakikisha teknolojia na elimu mpya vinafika kwa wakati, jambo litakaloongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.


Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Mlali, Amanda Hilary, amesema atahakikisha elimu hiyo inawafikia wakulima kupitia ngazi za kata na vijiji kwa kuendesha mafunzo na ziara za mashambani ili kuongeza uelewa wa mbinu bora za kilimo cha korosho.


Mwisho.

No comments: