![]() |
| Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Alnason Nguvila amesema umoja, ushirikiano, upendo na uelewa wa pamoja utatimiza adhma ya Serikali na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia |
Mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Alnason Nguvila amewasisitiza watendaji wa Serikali katika mkoa huo, kuanzia Sekretarieti ya Mkoa, halmashauri na Taasisi na Mashirika yote ya Umma, kufanya kazi kwa ushirikiano kisekta ili kutimiza adhma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Dkt. Nguvila ametoa rai hiyo, wakati akifungua kikao kazi cha robo ya mwisho, kilichowakutanisha Watendaji wa Serikali wa mkoa huo kutathmini utendaji wa shughuli wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Masai Land wilaya ya Arumeru leo Julai 17,2026.
"Lengo la kikao kazi hiki ni kutathmini utendaji wa shughuli za Serikali kwa Mkoa, kuona mafanikio na kubaini changamoto zilizojitokeza, utakaotoa dira na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa mwaka mpya wa fedha wa 2026/27, kukiwa na mipango thabiti na mwelekeo wa utekelezaji, kukiwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa watalamu wote.
Aidha, Dkt. Nguvila ameweka wazi kuwa, kikao hicho kitatumika kama sehemu ya kufahamiana na kutatua migongano na migogoro mbalimbali miongoni mwa washiriki wa Kikao hicho pamoja na kushughulikia kwa pamoja sintofahamu zilizopo baina ya Halmashauri, Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Taasisi za umma zilizopo katika Mkoa wa Arusha.
"Wakati mwingine hatufahamu hata mwelekeo wa uchumi kwenye Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla, hatuelewi masuala ya mfumuko wa bei, hatuelewi mipango ya Taifa ya uchumi ikoje hasa wakati huu ambapo tayari tumeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, yupo Mkurugenzi wa Benki Kuu BOT, tawi la Arushanatatufafanulia hali halisi ilivyo na sisi tunachangiaje katika kukuza uchumi." ameongeza kusema Dkt. Nguvila.
Awali Dkt. Nguvila amesisitiza suala la umoja, maelewano, upendo, dhamira ya dhati na kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya kila sekta na kufikia adhma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi na maono ya Mhe.Rais ya kurejesha tabasamu kwa wananchi.



No comments:
Post a Comment