![]() |
Mwandishi wetu Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utalii (Tanzania International Tourism Festival) linatarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu Jijini Arusha huku likiwa na lengo la kutangaza utalii, sanaa na utamaduni wa Tanzania pamoja na kufungua fursa mpya za biashara kwa wasanii na wadau wa sekta ya utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema Leo katika Hoteli ya Grand Mellia jijini Arusha, Mwanzilishi Mwenza wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Osman Yama, alisema tamasha hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, sanaa na utamaduni pamoja na chama cha TAFCA, kwa lengo la kuendeleza na kutangaza urithi wa Tanzania kupitia sanaa za uchongaji, uchoraji na ubunifu mwingine.
Yama alisema tamasha hilo litakuwa na shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya kazi za sanaa, warsha, mijadala ya kitaalamu pamoja na programu zitakazowapa wasanii uelewa kuhusu biashara ya sanaa, ulinzi wa kazi za ubunifu na fursa zilizopo katika masoko ya ndani na kimataifa.
Naye Rukia Welele, ambaye ni mdau katika sekta ya sanaa na utamaduni, alisema kuwa siku hiyo wasanii mbalimbali wataweza kuonesha kazi zao na wageni wengi kujifunza na kunufaika .
Rukia alisema kuwa sanaa si burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuelimisha jamii, kuhifadhi historia, na kuimarisha mshikamano wa kijamii kati ya mataifa mbalimbali.
Aliongeza kuwa wadau wote wanapaswa wanapaswa kutumia fursa hiyo ili kueneza kazi zao za sanaa ngazi ya kimataifa na kuongeza kipato chao.
Aidha alitoa wito kwa serikali na sekta binafsi kuwekeza zaidi katika vituo vya mafunzo ya sanaa, ili kuwajengea uwezo wasanii chipukizi na kuwasaidia kupata ujuzi wa kisasa.
Rukia alisisitiza kuwa sanaa ya Tanzania ina nafasi kubwa duniani endapo itawekewa mazingira mazuri ya kukuza vipaji na kuviunganisha na masoko ya kimataifa.


No comments:
Post a Comment