VIJANA WILAYANI IRAMBA, WAHIMIZWA UZALENDO NA KUSHIRIKI SHUGHULI ZA UJENZI WA TAIFA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 23 July 2026

VIJANA WILAYANI IRAMBA, WAHIMIZWA UZALENDO NA KUSHIRIKI SHUGHULI ZA UJENZI WA TAIFA

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Suleiman Yusuph Mwenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa Ujio wa Mwenge wa Uhuru Wilayani Iramba



SEIF TAKAZA, IRAMBA

maipacarusha20@gmail.com

Mkuu wa wilaya ya Iramba, Mkoani Singida, Alhaj Suleiman amewataka vijana nchini kuwa na uzalendo kwa kushiriki vema katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Yusuf Mwenda ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mjini Kiomboi.

Alhaj Mwenda amesema vijana wana wajibu mkubwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa, kwani wao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Vijana mnatakiwa kuwa na maono makubwa ya maisha na kuendelea kuwekeza katika elimu na ujuzi pamoja na kutumia uwezo wenu kuleta maendeleo yenu binafsi na jamii kwa ujumla” Alisisitiza Alhaj Mwenda.

Katika kongamano hilo vijana wamepatiwa elimu ya kutosha katika mada mbalimbali na kuwajengea uwezo wa uzalendo na maadili mema, pamoja na kuwahimiza kushiriki kikamilifu ujenzi wa Taifa.

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya vijana wilaya ya Iramba Peterson Anton Ngahava amesema zaidi ya vijana 570 wameshiriki kongamano hilo ambapo vijana walielezwa mada kadhaa pamoja na elimu ya kupambana na rushwa iliyotolewa na Michael Ngomo Afisa Uchunguzi wa Takukuru wilaya ya Iramba.

Elimu ya mapambano dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya iliyotolewa na Mkaguzi wa Polisi Thomas Chalamila, mada nyingine ilikuwa kujenga amani, umoja na upendo katika jamii na kuheshimu utawala wa kisheria imetolewa na Mkufunzi Neema Samwel kutoka Open University tawi la Singida, elimu ya uraia, mshikamano wa kitaifa, uzalendo na kujitolea kwa ajili ya Taifa ambayo ilitolewa na Levina Kavishe kutoka Open University tawi la Singida, mada nyingine ilikuwa kuibua na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika mazingira yanayowazunguka vijana ambayo ilitolewa Abraham Mtongole kutoka Harvetas Dodoma.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa wilaya amesema maandalizi ya ujio wa mwenge wa uhuru wilayani Iramba yamekamlika.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Alhaj Mwenda amesema wilaya hiyo ina miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya bilioni kumi na mbili (12) ambayo ni ya kuona, kuzindua na kuweka mawe ya msingi.

“Mwenge wa Uhuru tutaupokea Julai 24 2026 katika kijiji cha Ndulungu ukitokea Wilaya ya Singida ambapo mkesha utakuwa katika kijiji cha Misigiri katika viwanja vya shule ya msingi Misigiri” Alieleza Alhaj Mwenda

Alisema miradi hiyo ni pamoja na Ofisi ya Kijiji Ndulungu, Zahanati ya Urughu, Skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Masimba, kikundi cha vijana Nguvumali Ndago, Kiwanda cha kusindika mafuta ya Alizeti, Ukumbi wa mikutano na nyumba ya kulala wageni ya mwananchi Ndago, ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari Kizaga, Utengenezaji wa Thamani shule ya sekondari Kizaga, uhifadhi wa mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 20 katika kijiji cha Masagi.

MWISHO

No comments: