![]() |
| Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Iramba Alhaj Suleiman Mwenda katika kikao kazi |
SEIF TAKAZA IRAMBA
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Wilaya ya Iramba, Alhaj Suleiman Mwenda, amewataka watumishi wa umma katika Wilaya ya Iramba kuziishi na kuzitekeleza falsafa nne (4) za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili kuchochea ufanisi wa utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alhaj Mwenda ameyasema hayo tarehe 12 Agosti, 2026, wakati akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa umma wa Wilaya ya Iramba kilichofanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri.
Katika kikao hicho, Mwenda amewataka watumishi kuziishi falsafa hizo ambazo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya. ili kuhakikisha matokeo ya falsafa hizo yanaonekana katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan kupitia uwajibikaji, ushirikiano, uadilifu na utoaji wa huduma zenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.
“Sisi kama watumishi lazima tuhakikishe tunaziishi na kuziendeleza falsafa hizi katika majukumu yetu ya kila siku.” Amesema Mwenda
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu, Ndg. Elikana Zabron, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, amesema Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Idara na Vitengo mbalimbali, itayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa katika kikao hicho kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kikao kazi hicho kililenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, Idara na Vitengo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Kujadili muelekeo na mpango wa Taasisi hizo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na miaka mitano ijayo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao.
MWISHO

No comments:
Post a Comment