IRAMBA: MWENYEKITI WA HALMASHAURI AHIMIZA UWAJIBIKAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2026/2027 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 30 August 2026

IRAMBA: MWENYEKITI WA HALMASHAURI AHIMIZA UWAJIBIKAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2026/2027

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi  akifunga Kikao cha Baraza la Madiwani


 SEIF TAKAZA IRAMBA


maipacarusha20@gmail.com 


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na Diwani wa Kata ya Kyengege Mhe. Innocent Msengi, amewataka viongozi na watendaji Iramba kuongeza uwajibikaji katika kusimamia majukumu waliyopewa, ili kuhakikisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.


Ametoa wito huo tarehe 28 Agosti, 2026, katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kikao cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika Ukumbi Mkubwa wa halmashauri, akisisitiza umuhimu wa kila kiongozi na mtendaji kutimiza wajibu wake kwa uadilifu, weledi na kuzingatia mipango iliyowekwa na Halmashauri.


“kwa bajeti hii ambayo tumekwisha ianza, kila mmoja akafanye kazi, kila mmoja akasimamie shughuli ambazo tumejipangia” amesema


Aidha, amepongeza jitihada zinazofanywa na viongozi pamoja na watendaji, kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapata chakula cha mchana shuleni, kwani mpango huo unaongeza mahudhurio, utayari wa kujifunza na hivyo kuchangia kuimarika kwa ufaulu.


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ndg. Morton Msowoya kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, ameahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na Baraza la Madiwani, kwa lengo la kuboresha utendaji na kuhakikisha Halmashauri inasonga mbele kimaendeleo katika sekta mbalimbali.


Katika kikao hicho, Waheshimiwa madiwani wametoa maoni, kuuliza maswali na kutoa mapendekezo yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa shughuli za Halmashauri na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba.

No comments: