Mwandishi wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Goodluck Medeye, amefanikisha kupatikana kwa shilingi milioni 14 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la KKKT Ushirika wa Manyire, huku akiwapongeza viongozi na waumini wanaoendelea kujitoa kwa maendeleo ya nyumba ya ibada.
Akizungumza kanisani hapo, Medeye alisema anafurahishwa na mwitikio mkubwa wa waumini na viongozi waliojitokeza kushiriki harambee hiyo, lakini alimpongeza kwa namna ya kipekee Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, kwa moyo wake wa kujitolea na kuunga mkono shughuli za maendeleo.
Alisema Mrema ameonyesha mfano wa uongozi unaotanguliza matendo kuliko maneno, akieleza kuwa amekuwa akimtumikia Mungu kwa vitendo kupitia ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za kijamii na kidini.
Medeye aliongeza kuwa viongozi wengine wanapaswa kuiga mfano huo wa kujitoa kwa maendeleo ya jamii na taasisi za dini, akisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi na wananchi ndiyo msingi wa mafanikio ya miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, ambaye alihudhuria ibada hiyo akiwa ameambatana na mke wake, alisema viongozi wanaochangia harambee za ujenzi wa makanisa wanafanya jambo la muhimu linalostahili kuungwa mkono.
Mrema alisema yeye na familia yake wameamua kushiriki kwa awamu tatu katika kuchangia ujenzi wa kanisa hilo ili kuhakikisha wanatoa mchango endelevu kwa kazi ya Mungu.
"Leo nina kiasi katika bahasha na sitakitaja hadharani Pia nitaweka kiasi kama hiki katika akaunti ya kanisa, na mwisho wa wiki nitashirikiana na mke wangu kuangalia kiasi kingine kama pato letu la familia," alisema Mrema.
Alisema ameweka utaratibu binafsi wa kutotangaza hadharani kiasi cha fedha anachochangia, akieleza kuwa kufanya hivyo kunawapa nafasi watu wote kushiriki kwa uwezo wao bila kujihisi kutengwa au kushushwa hadhi.
Naye mmoja wa waumini wa KKKT Ushirika wa Manyire alisema Mrema amekuwa mstari wa mbele kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo ya wananchi, iwe wakati wa shida au wa furaha.
Waumini hao walieleza kuwa uongozi wa aina hiyo unapaswa kuigwa na viongozi wengine, wakisema kujitoa kwa vitendo na kuwa karibu na wananchi ndiko kunakojenga imani na kuharakisha maendeleo ya jamii


No comments:
Post a Comment