Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Benki ya PBZ imeahidi kuendelea kupanua huduma zake za kifedha kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Uwezeshaji wa Mikopo wa PBZ na Msimamizi wa Masoko Kanda ya Morogoro, **Mohamed Kaiza Makame**, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha, **Laurent Deogratius Luswetula**, aliyetembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro.
Makame alisema PBZ imeendelea kupata mwitikio mzuri kutoka kwa wananchi wa Morogoro tangu ilipoanza kutoa huduma zake mkoani humo mwaka 2024, huku ikiongeza kuwa benki hiyo imefanikiwa kujijengea imani kwa wateja wake.
*"PBZ tumejiwekeza moja kwa moja na tunalitambua soko. Ndani ya kipindi cha miaka miwili tumefanya biashara nzuri na wananchi wa Morogoro pamoja na mikoa jirani,"* alisema Makame.
Aliongeza kuwa PBZ ina uzoefu mkubwa katika sekta ya fedha na itaendelea kusogeza huduma zake katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwawezesha wananchi kukuza uchumi wao na kuongeza mitaji ya biashara.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na taasisi za kifedha ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Luswetula pia alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira, akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda miti kwa wingi.
*"Kila mwananchi ana wajibu wa kutunza mazingira. Ni muhimu kuendelea kupanda miti na kulinda mazingira yetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,"* alisema.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, hatua ambayo itachochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
Mwisho..


No comments:
Post a Comment