Rais Samia ziarani nchini Angola kwa siku mbili - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 1 August 2026

Rais Samia ziarani nchini Angola kwa siku mbili

 

 


RAIS Samia akiagana na baadhi ya viongozi 


Rais Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31, 2026 ameondoka nchini kuelekea Angola kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kwa mwaliko wa Rais wa Angola, João Lourenço.


Akiwa nchini humo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki hafla ya uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyojengwa jijini Luanda. 

Uzinduzi huo utafanyika kwa ushirikiano na mwenyeji wake, Rais Lourenço.


Hafla hiyo pia itawakutanisha viongozi mbalimbali pamoja na familia ya Baba wa Taifa, ikiongozwa na Mama Maria Nyerere kama sehemu ya kutambua na kuenzi mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika harakati za ukombozi wa Afrika na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Angola.


Mbali na kushiriki uzinduzi wa hospitali hiyo, Rais Samia atafanya mazungumzo ya kikazi na Rais Lourenço kuhusu namna ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali yenye maslahi kwa nchi hizo mbili.


Ratiba ya ziara hiyo pia inajumuisha ushiriki wa Rais Samia katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na wake wa marais wa Afrika. Hafla hiyo inalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa programu za kijamii na kiuchumi zinazowalenga wanawake na vijana barani Afrika.


Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, ambao ulijengwa wakati wa harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika na umeendelea kuimarishwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili.

No comments: