Rombo yaweka mkazo usalama barabarani, madereva bodaboda wakabidhiwa vyeti vya udereva - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 16 August 2026

Rombo yaweka mkazo usalama barabarani, madereva bodaboda wakabidhiwa vyeti vya udereva





Na Mwandishi wetu, 


maipacarusha20@gmail.com 


Rombo. Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amechukua hatua za kuimarisha usalama barabarani wilayani humo kwa kuwawezesha waendesha pikipiki (bodaboda) kupata mafunzo ya udereva na vyeti vinavyowawezesha kuomba leseni.


Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa wa sheria na matumizi salama ya barabara, pamoja na kupunguza ajali zinazohusisha pikipiki katika wilaya hiyo.


Akizungumza leo wakati wa kukabidhi vyeti kwa Maofisa usafirishaji 70 tarafa ya Mengwe, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Rombo, Mohammed Semfuko, amesema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ajali, nyingi zikihusisha pikipiki.


“Namshukuru sana Mbunge wetu, Profesa Adolf Mkenda, kwa kuliona hili. Wilaya yetu ina changamoto ya ajali ambazo mara nyingi husababishwa na pikipiki. Hii inatokana na baadhi ya waendesha pikipiki kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi sahihi ya barabara na vyombo vya usafiri,” alisema.


Semfuko amesema takwimu zilizofanywa na Jeshi la Polisi zilionyesha kuwa Rombo ina vituo 54 vya bodaboda vyenye jumla ya waendesha pikipiki 480.


Aamesema lengo la zoezi hilo lilikuwa kubaini idadi ya waendesha pikipiki wenye elimu ya usalama barabarani pamoja na leseni za udereva, ambapo ilibainika kuwa ni wachache waliokuwa na sifa hizo.


“Tunamshukuru mbunge kwa kuliona hili na kuamua kufanya jitihada za kuwawezesha kupata vyeti ambavyo vitawasaidia kupata leseni za udereva na hivyo kusaidia kupunguza ajali za barabarani,” alisema.


Semfuko pia aliwataka waendesha pikipiki kutumia vifaa vya usalama vilivyowekwa kwenye vyombo vyao na kuacha kuviondoa au kuvibadilisha kwa vifaa visivyokidhi viwango.


“Pikipiki zinapokuja zinakuja na vifaa vyake, kwa mfano taa kubwa. Wengi wanaziondoa na kuweka taa ndogo, jambo ambalo ni hatari. Pia kuna michezo mnayoifanya barabarani ambayo inaweza kuhatarisha maisha. Mnafanya vitendo ambavyo mwisho wa siku vinaweza kusababisha madhara,” alisema.



Akizungumza, Mwakilishi wa Mbunge wa Rombo, Temmy Masae, aliwataka vijana wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria kwa pikipiki kuthamini kazi hiyo na kuendelea kuifanya kwa kuzingatia sheria na usalama.


“Vijana ndio uti wa mgongo wa nchi yoyote. Nawashauri vijana wenzangu kuendelea kujituma kwa kujiajiri na kulisha familia zenu kupitia kazi halali ya usafirishaji wa abiria. Asiwepo mtu anayewadharau kwa kufanya kazi hii,” alisema.


Alisema waendesha bodaboda wana mchango mkubwa katika kurahisisha shughuli za usafirishaji na kukuza uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.


Masae pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha vijana kuwa karibu na viongozi wa Serikali na kupata fursa za elimu na ushauri kuhusu shughuli zao.


“Ni ndoto ya Mbunge wa Rombo kuhakikisha maofisa usafirishaji wote ndani ya Wilaya ya Rombo wanafanya kazi katika mazingira salama na wanapata leseni zitakazowawezesha kufanya kazi sehemu yoyote Tanzania,” alisema.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodaboda Kata ya Mamsera Kati, Gofari Masae, alisema kazi ya usafirishaji imekuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa vijana wengi katika eneo hilo.


“Kazi hii imekuwa ajira kwetu kwa sababu tunapata kipato kwa ajili ya kutunza familia zetu. Hapa pia tumenufaika na mikopo ya asilimia 10 ya vijana inayotolewa na halmashauri yetu,” alisema.


Kaimu Ofisa Tarafa ya Mengwe, Rombo, Msuya Bakari, amesema baadhi ya vijana hao wameweza kunufaika na mikopo ya halmashauri iliyowawezesha kupata pikipiki kwa ajili ya shughuli za usafirishaji.


“Vijana hawa wamenufaika na mikopo ya halmashauri. Wameweza kupata mikopo ya pikipiki kwa ajili ya shughuli za usafirishaji. Tunashukuru Jeshi la Polisi na Serikali kwa kutoa elimu kwa vijana wetu kuhusu namna ya kujilinda wao pamoja na abiria wanaowasafirisha,” alisema.



Naye, Katibu wa Mbunge wa Rombo, John Mrina, aliwataka waendesha pikipiki kuhakikisha wanakamilisha taratibu muhimu za kupata nyaraka zinazohitajika ili kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.


Aliwataka ambao hawajapata namba za Taifa za Utambulisho (NIDA) kuhakikisha wanazipata na kisha kufuata taratibu za kupata namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Amesema hatua hiyo, itasaidia waendesha pikipiki kutekeleza shughuli zao za usafirishaji kwa kuzingatia matakwa ya sheria na taratibu za Serikali.



Mwisho.

No comments: