![]() |
| Gari la wagonjwa ambalo limekabidhiwa hospitali ya Huruma, wilaya ya Rombo |
![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akikabidhi ufunguo wa gari la wagonjwa kwa Daktari kiongozi wa hospitali ya Huruma, Sista Dk Daria Mushi |
Mwandishi wetu, Rombo
maipacarusha20@gmail.com
Rombo. Serikali imetoa gari jipya la kubeba wagonjwa kwa Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni utekelezaji wa ombi lililowasilishwa na viongozi wa hospitali hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Gari hilo limekabidhiwa kwa niaba ya Waziri wa Afya, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia ombi hilo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema hatua hiyo inaonesha namna serikali ya awamu ya Sita inavyoendelea kusikiliza na kutekeleza mahitaji ya wananchi.
“Tulifanya ziara pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Afya, ambapo viongozi wa hospitali waliwasilisha maombi mbalimbali. Miongoni mwa maombi hayo lilikuwa ni gari la kubeba wagonjwa. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa gari hili jipya kabisa kwa ajili ya Hospitali ya Huruma,” amesema RC Babu
RC Babu amesema gari hilo litasaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa, hususan katika usafirishaji wa wanaohitaji huduma za matibabu katika vituo vya afya vyenye uwezo mkubwa zaidi.
Pia amesema kuwa maendeleo yaliyofikiwa na Hospitali ya Huruma yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Mbunge wa Jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda, akisema amekuwa akishirikiana na Serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya jimbo hilo.
“Niungane na wenzangu kumshukuru sana Mbunge wa Jimbo hili, Profesa Adolf Mkenda, kwa kazi nzuri anayoifanya hapa Rombo. Mheshimiwa Mkenda anafanya kazi nzuri sana na kazi anazozifanya zinaonekana,” amesema RC Babu
Akizungumza Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Rombo, Masoud Melimeli amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeendelea kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa maeneo mbalimbali, jambo ambalo limewezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunaifurahia kazi anayofanya Profesa Mkenda kwa sababu ametengeneza mahusiano mazuri sana Rombo. Ukiangalia uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Kilimanjaro na wilayani, unamkuta Profesa Mkenda. Ni uteuzi mzuri ambao Mheshimiwa Rais amefanya, na kazi anazozifanya zinaonekana,” alisema.
Kwa mujibu wa Melimeli, makabidhiano ya gari hilo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na miundombinu inayokidhi mahitaji yao.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa kisiasa na wananchi unapaswa kuendelea kuimarishwa ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya gari hilo, Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Huruma, inayomilikiwa na watawa wa Kanisa Katoliki, Dk Daria Mushi, amesema uongozi wa hospitali hiyo umepokea msaada huo kwa furaha na shukrani kubwa.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia gari hili. Kwetu sisi ni msaada mkubwa sana kwa sababu litatusaidia katika kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji huduma za juu zaidi katika hospitali nyingine, pamoja na shughuli nyingine za huduma za afya,” alisema.
Alisema msaada huo ni ushahidi wa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na taasisi za dini katika kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Dk Daria pia aliwashukuru viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha upatikanaji wa gari hilo, akiwemo Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, kwa mchango wake katika kuendeleza huduma za afya na maendeleo ya hospitali hiyo.
“Tunawashukuru viongozi wetu wote ambao wamekuwa wakisimamia na kufikisha mahitaji yetu kwa Serikali. Tunamshukuru sana Profesa Adolf Mkenda kwa namna ambavyo amekuwa karibu na hospitali na kusaidia kusukuma masuala mbalimbali ya maendeleo,” alisema.
Alisema gari hilo jipya litapunguza changamoto za usafirishaji wa wagonjwa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, huku akiahidi kuwa hospitali hiyo italitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment