SHIBUDA AMSHAURI NCHIMBI AJITAFAKARI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 26 August 2026

SHIBUDA AMSHAURI NCHIMBI AJITAFAKARI

 


Na Mwandishi Wetu


maipacarusha20@gmail.com 


MWANACHAMA mkongwe wa TANU na CCM na Mbunge mstaafu wa Maswa, Mzee John Magale Shibuda maarufu ‘Drogba’, amemtaka Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, kujitafakari kati ya mambo mawili kujiuzulu kwa heshima kama alivyofanya John Samwel Malecela na kubaki ndani ya chama akiwa amelinda jina na historia yake, au kusubiri chama kimfanyie uamuzi kama Aboud Jumbe na ilivyowakuta vigogo wengine waliowahi kuingia katika mvutano mkubwa na TANU na baadaye CCM. 


Shibuda amesema historia inayopaswa kumsaidia Nchimbi kujitafakari inaanzia kwa Oscar Kambona, aliyekuwa kigogo wa TANU lakini alipotofautiana na mwelekeo wa chama mwaka 1967 akaondoka nchini kwenda Uingereza, Aboud Jumbe, ambaye mwaka 1984 mvutano kuhusu Muungano uliishia kuondoka kwake katika Urais wa Zanzibar na nafasi nyingine za juu na Horace Kolimba, Katibu Mkuu wa CCM aliyekumbana na mvutano mkubwa ndani ya chama.


Upande mwingine yupo John Samwel Malecela, ambaye alipofika katika mazingira magumu mwaka 1994 aliondoka Uwaziri Mkuu lakini akaendelea kubaki ndani ya CCM na baadaye kuendelea kushika nafasi za juu katika chama.


Shibuda anaeleza kuwa "mifano haikuishia hapo wapo wakina Augustine Mrema waliondoka CCM kuelekea NCCR-Mageuzi na kujaribu kuingia Ikulu mwaka 1995 bila kufanikiwa, Edward Lowassa alipoondoka CCM mwaka 2015 akaenda CHADEMA na kugombea urais, hakufanikiwa kuiondoa CCM madarakani na baadaye akarejea chama hicho". Amesema


Ameongeza kwa kukumbushia ya  Bernard Membe kuondoka CCM na kuwania urais kupitia ACT-Wazalendo mwaka 2020 bila kufanikiwa ambapo kwa mujibu wa mzee Shibuda, matukio hayo yalitokea katika mazingira tofauti lakini ni somo kwa Nchimbi kuwa vigogo wengi waliowahi kuingia katika mapambano makubwa na chama cha Mapinduzi walishindwa kupata matokeo waliyotarajia.


Shibuda amesema Nchimbi ana sababu zaidi ya kuisoma historia hiyo kwa sababu yeye mwenyewe tayari aliwahi kukutana na mkono wa nidhamu wa CCM, Mwaka 2015, Nchimbi pamoja na Adam Kimbisa na Sophia Simba walipinga hadharani uamuzi wa Kamati Kuu baada ya Edward Lowassa kuondolewa katika mchakato wa wagombea urais; mwaka 2017 CCM ikampa Nchimbi onyo kali na kumzuia kugombea nafasi yoyote ndani ya chama kwa miaka minne, hatua iliyoelezwa kuwa ilihusiana na mwenendo wake katika uchaguzi wa 2015.


Kwa mujibu Shibuda, Malecela na Jumbe wanakuwa njia mbili muhimu za  Nchimbi kujitafakari. 


Amesema Malecela aliachia nafasi yake katika mazingira magumu lakini akabaki na chama na kuendelea kuwa sehemu ya historia yake, wakati Jumbe alifika mwisho wa mvutano akiwa kwenye kilele cha madaraka na akaondoka katika nafasi zake. 


“Nchimbi ajitafakari kati ya mawili, ajiweke kando kwa heshima, alinde jina lake, imani yake kwa CCM na historia ya kizazi chake kama Malecela au asubiri chama kimfanyie uamuzi kama ilivyowakuta kina Jumbe. historia ipo mbele yake, na yeye mwenyewe tayari ana uzoefu wa mwaka 2015 na adhabu ya 2017. Sasa ni wakati wa kuchagua namna anavyotaka historia yake iandikwe,” amesema Shibuda.

No comments: