THRDC WALITAKA JESHI LA POLISI DSM KUMUACHIA KWA DHAMANA WAKILI MADELEKA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 15 August 2026

THRDC WALITAKA JESHI LA POLISI DSM KUMUACHIA KWA DHAMANA WAKILI MADELEKA


Wakili Peter Madeleka



Mwandishi Wetu maipac


maipacarusha20@gmail.com


Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumwachia huru mara moja kwa dhamana Wakili Peter Madeleka, ukisisitiza kuwa tuhuma zinazomkabili zina dhamana kisheria na lazima Katiba iheshimiwe.


Wito huo umetolewa leo Agosti 15, 2026, na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, kufuatia hatua ya polisi kumkamata Madeleka kwa madai ya kudharau amri za Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi zilizotolewa mnamo Julai 27 na Agosti 13, 2026.


THRDC imekumbusha kuwa Ibara ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inalinda kwa dhati haki ya kila mtu kuwa huru, na kwamba hatua yoyote ya kisheria dhidi ya raia haipaswi kuingilia msingi huo wa kikatiba bila sababu za kisheria.


"Kwa kuwa Wakili Madeleka yupo chini ya ulinzi wa Polisi na tuhuma zinazomkabili zinadhaminika, THRDC inatoa wito kwa Jeshi la Polisi kumwachia huru kwa dhamana ya Polisi bila kuchelewa, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kwa mujibu wa sheria," amesisitiza Wakili Olengurumwa.


Mtandao huo pia umeshinikiza Jeshi la Polisi kutoleta vikwazo na badala yake uhakikishe Wakili Madeleka anapewa haki yake ya kikatiba ya kuonana na mawakili wake pamoja na familia yake, huku akifahamishwa kikamilifu msingi wa kisheria wa kukamatwa kwake.


Shinikizo hilo la THRDC linakuja huku kukiwa na muungano mkubwa wa taasisi za sheria na haki za binadamu nchini zinazotaka kuona utawala wa sheria na utu ukizingatiwa bila ukiukaji wowote.

No comments: