![]() |
| Wakili Peter Madeleka |
Mwandishi Wetu maipac
maipacarusha20@gmail.com
Wakili wa Kujitegemea, Peter Madeleka, ameachiwa kwa dhamana leo Agosti 17, 2026, baada ya kushikiliwa kwa takriban siku tatu katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) Dar es Salaam.
Upatikanaji wa dhamana hiyo umethibitishwa na Wakili Paul Kisabo kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambaye amekuwa akifuatilia mchakato huo tangu asubuhi ya leo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kisabo ameeleza kuwa licha ya Wakili Madeleka kutofikishwa mahakamani ndani ya saa 24 kama sheria inavyoelekeza, Jeshi la Polisi limeridhia kumpa dhamana.
Akielezea mchakato wa kuachiliwa kwake, Wakili Kisabo amesema: “Asubuhi niliamkia Central Policy Station Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia dhamana yake. Na baada ya kufika nilikutana na ZCO na kuzungumza naye kuomba dhamana ya wakili Madeleka lakini yeye ZCO aliniambia nirudi mchana saa 8” Alisema wakili Kisabo
Baada ya kurejea kituoni hapo majira ya mchana, taratibu za dhamana zilikamilika kwa Madeleka kudhaminiwa na watu watatu. “Amekubali kwamba Madeleka adhaminiwe na watu watatu tumemdhamini kwa maana ya mimi Paul Kisabo nimemdhamini pamoja na ndugu zake wengine wawili... dhamana iko wazi na tumemdhamini,” ameongeza Wakili Kisabo.
Kuhusu utaratibu wa kumfikisha mahakamani, Wakili Kisabo amebainisha kuwa msisitizo wao kwa sasa ulikuwa ni kupata dhamana ya polisi ili mteja wao aweze kuwa nje wakati taratibu zingine zikiendelea.
Wakili Peter Madeleka alikamatwa Agosti 14, 2026, majira ya saa 9:30 alasiri akiwa katika viunga vya Mahakama ya Uhujumu Uchumi (Mikocheni B) wakati akitekeleza majukumu yake ya kitaaluma. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Madeleka alishikiliwa kwa tuhuma za kudharau amri za Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi zilizotolewa tarehe 27 Julai na 13 Agosti, 2026.
Ukamataji huo ulitokea saa chache baada ya Madeleka kutangaza nia ya kufungua kesi kupinga zuio la Msajili wa Mahakama Kuu linalowazuia mawakili kufanya mahojiano na vyombo vya habari ndani ya maeneo ya mahakama.

No comments:
Post a Comment