Wakulima 100,000 Wanufaika na Mafunzo ya TAHA Kuongeza Thamani ya Mazao - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 7 August 2026

Wakulima 100,000 Wanufaika na Mafunzo ya TAHA Kuongeza Thamani ya Mazao



Na Mwandishi wetu, Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Zaidi ya wakulima 100,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefanikiwa kupata elimu  ya kilimo bora cha mazao ya mbogamboga, hususan vitunguu na nyanya, kupitia (TAHA), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao hayo.


Elimu hiyo imetolewa moja kwa moja kwenye kongani za wakulima, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija na kuwafanya wazalishe mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.


Akizungumza kuhusu mafanikio ya programu hiyo, Afisa Kilimo wa TAHA, Mganga Christopher, alisema elimu hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima wengi, hasa katika uzalishaji wa zao la kitunguu.


Alisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, zao la kitunguu kwa sasa lina thamani kubwa sokoni kutokana na wakulima wengi kuzingatia kanuni na mbinu bora za uzalishaji.


"Baadhi ya mambo muhimu tunayosisitiza ni matumizi ya mbegu bora, kufuata viwango sahihi vya matumizi ya viuatilifu na mbolea, pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kupata mazao yenye ubora wa hali ya juu," alisema.



Mganga aliongeza kuwa wakulima watakaoendelea kutumia mbinu hizo wataongeza ushindani wa mazao yao katika masoko ya kimataifa, ambapo mahitaji ya vitunguu kutoka Tanzania bado ni makubwa.


Alitaja Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kuwa miongoni mwa nchi zinazotegemea kwa kiasi kikubwa vitunguu vinavyozalishwa nchini Tanzania.


Aidha, aliwahimiza wakulima wa vitunguu na nyanya kujiunga na TAHA ili waweze kupata elimu endelevu, taarifa za masoko pamoja na fursa mbalimbali za kuuza mazao yao ndani na nje ya nchi.

No comments: