
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima
Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WANAFUNZI takribani 6,800 kutoka nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na wenyeji Tanzania wanatarajiwa kushiriki Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) 2026, yanayotarajiwa kufanyika katika Mkoa wa Morogoro.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 12 hadi 23, 2026 katika Manispaa ya Morogoro.
Kwa upande wa Tanzania, jumla ya wanafunzi 1,510 kutoka mikoa 26 wanatarajiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo, hali ambayo inaweka rekodi ya idadi kubwa ya ushiriki wa Tanzania katika historia ya mashindano ya FEASSA.
Mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya 23 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiwa mwenyeji kwa mara ya tano na ni mara ya kwanza kwa Mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, FEASSA ni mashindano makubwa ya michezo kwa wanafunzi katika ukanda wa Afrika Mashariki, yenye lengo la kukuza vipaji vya vijana katika michezo, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji maalum.
Aidha, mashindano hayo yana nafasi muhimu katika kujenga umoja, mshikamano, urafiki na mahusiano mema miongoni mwa vijana wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika mashindano hayo, jumla ya michezo 20 itashindaniwa kwa upande wa shule za sekondari, michezo sita (6) kwa shule za msingi, pamoja na michezo minne (4) kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mkoa wa Morogoro umejipanga kikamilifu kuhakikisha unakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo, ambapo jumla ya viwanja 21 ndani ya Manispaa ya Morogoro vitatumika katika mashindano hayo.
Aidha, maeneo manane (8) yametengwa kwa ajili ya malazi ya wanafunzi watakaoshiriki mashindano hayo.
Mkuu wa Mkoa amesema maandalizi yamezingatia maeneo muhimu ikiwemo usalama, afya, usafi wa mazingira, usafiri, chakula, malazi na huduma nyingine muhimu, huku Serikali kupitia Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiendelea kuhakikisha kila eneo linakuwa tayari kabla na wakati wa mashindano.
Mashindano ya FEASSA 2026 yanatarajiwa kuwa zaidi ya tukio la michezo, kwani yanatoa fursa kubwa kwa wananchi wa Morogoro kunufaika kiuchumi, kiutalii na kiutamaduni.
Kuwapo kwa maelfu ya wanafunzi, walimu, viongozi, waamuzi na wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kunatarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wafanyabiashara na watoa huduma katika sekta za usafiri, chakula, malazi, bidhaa mbalimbali na huduma nyingine.
Aidha, wageni watapata fursa ya kuifahamu zaidi Morogoro, ikiwemo vivutio vyake vya utalii, pamoja na utamaduni na ukarimu wa wananchi wa Mkoa huo.
Mashindano hayo pia yanatarajiwa kutoa fursa ya mabadilishano ya kiutamaduni miongoni mwa vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki, hatua ambayo itasaidia kuimarisha uhusiano na mshikamano wa kikanda.
Mashindano ya FEASSA 2026 yataanza rasmi Agosti 12, 2026, huku hafla ya ufunguzi rasmi ikitarajiwa kufanyika Agosti 16, 2026.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk Mwigulu Nchemba.
Mashindano hayo yatahitimishwa Agosti 23, 2026, yakitarajiwa kuwakutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki katika michezo, kujenga urafiki na kuimarisha mshikamano wa kikanda.
Mwisho..
No comments:
Post a Comment