30 wachaguliwa kuongoza Burunge WMA. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 18 September 2026

30 wachaguliwa kuongoza Burunge WMA.

 

Viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza burunge WMA kutoka kijiji cha Olasit



Wanavijiji Wakipiga kura burunge WMA



Mussa Juma, MAIPAC 


maipacarusha@gmail.com


Halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini, Mkoa wa Manyara imekamilisha uchaguzi wa viongozi 30 ambao wataongoza Jumuiya ya hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge.


Viongozi hao 30, wamechaguliwa kutoka katika vijiji 10 ambavyo vinaunda Jumuiya hiyo ambapo kila Kijiji kimechagua viongozi watatu.


Akizungumza Jana wakati akihitimisha uchaguzi katika Kijiji cha Olasiti, Kwa Niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Afisa wanyapori wa wilaya Babati, Christopher Laizer alisema uchaguzi huo unafanyika baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza Muda wao.


Laizer alisema kabla ya viongozi hao kumaliza Muda mwezi June mwaka huu, walikuwa wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali.


"Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Mkurugenzi wa halmashauri ndiye anawajibu wa kuitisha na kusimamia uchaguzi Jambo ambalo limekamilika "alisema 

Upigaji kura ukiendelea

Katika uchaguzi uliofanyika Kijiji cha Olasiti viongozi waliochaguliwa ni Ngotei Lomayani aliyepata kura 153 ,Fred Saitabau (84)na loseku Sanin'go (169) baada ya kuwashinda wagombea 10 waliokuwa wamejitokeza.


Wakizungumza baada ya kuchaguliwa viongozi hao wapya waliahidi kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha Burunge WMA inaendelea kuwa bora nchini.


Lomayani alisema suala la kuongeza mapato na kupunguza migogoro baina ya Wanyamapori na wananchi watalipa uzito.

Wananchi wakiwa katika uchaguzi wa WMA burunge

Baada ya kukamilika uchaguzi huo wa wajumbe kutoka vijijini(AA) kati yao watamchagua Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na vile vile itachaguliwa Bodi ya kusimamia Jumuiya hiyo.


Diwani wa Kata ya Ngaiti, Stevin Mollel alisema viongozi hao wapya wanatakiwa kusaidia Burunge WMA kuwa bora Afrika.


Mollel alisema kwa sasa mapato kwa mwaka yamefikia billioni  4 hivyo uongozi Mpya unapaswa kuongeza mapato hayo.

Diwani Stevin Mollel.akizungumza uchaguzi burunge WMA

"Tunawataka wasirudie kuleta migogoro ambayo ilisababisha kusimamishwa viongozi wote waliopita, tunaimani kubwa sasa kwani viongozi wengi waliochanguliwa ni sura mpya"alisema.


Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Anna Mbogo alisema uchaguzi huo umefanyika baada ya kukamilika maboresho ya Katiba na Mfumo wa uendeshaji.


Burunge WMA ipo Kati Kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na hivyo kuifanya kuwa katika eneo muhimu nchini la kiikolojia.


Mwisho

No comments: