Andikeni habari za uchunguzi juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuleta uwajibikaji - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 25 September 2026

Andikeni habari za uchunguzi juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuleta uwajibikaji



Mwandishi wetu,Dodoma


maipacarusha20@gmail.com


Waandishi wa habari za mazingira nchini, wametakiwa kuandika kwa kina habari za uchunguzi juu ya mambo yanayoendelea nchini ambayo yanachangia  athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuokoa jamii.


Maeneo mengi nchini, yanaendelea kuathirika na athari ya mabadiliko ya tabianchi, kutokana na kuendelea ukataji wa miti, upanuzi wa mashamba maeneo yaliyohifadhiwa, uvamizi wa vyanzo vya maji, uchafu wa mazingira, uvamizi wa maeneo ya nyanda za malisho na uchimbaji madini ambayo haujali athari za kimazingira.

Mhariri  mwandamizi wa habari za mazingira Deodatus Mfugale.

Mhariri  mwandamizi wa habari za mazingira, Deodatus  Mfugale akitoa mada ya habari za  uchunguzi wa mazingira, katika mafunzo ya wanahabari 35 wa mikoa ya kanda ya kati, jijini Dodoma, mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu (THRDC) na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) kwa udhamini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO).


Mfugale alisema, Wanahabari wana nafasi ya kuokoa jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchini, kwa kuandika na kuibua mambo ambayo yanachochea uharibifu wa mazingira kwa kutumia kwa usahihi na kutumia takwimu sahihi, sheria na hivyo kuibua uwajibikaji .


"Waandishi nendeni mkaandike habari za uchunguzi kusaidia jamii ili kuifanya dunia kuendelea kuwa salama lakini muandike kwa usahihi  na kujumuisha sauti za wananchi wanaoathirika"anasema.

Mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma akiwasilisha mada 

Mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma akitoa mada ya msingi wa habari za mazingira alisema mwandishi wa habari za mazingira  anapaswa kuandika kwa usahihi,kuandika kwa uhuru,kuelewa maudhui ya jambo ambalo anataka kuliandika, kushirikisha sauti za makundi yote katika jamii ikiwepo Wanawake, vijana, kuleta uwajibikaji na kutetea maslahi ya umma.


Juma alisema wanahabari wanapaswa kuchunguza zaidi athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika maeneo mbalimbali, ambazo zimetokana na ongezeko la joto duniani,Ukame, Mafuriko,upungufu wa uzalishaji wa chakula,uharibifu wa ikolojia.

 Mkurugenzi  wa Miradi na Uendeshaji wa (THRDC), Wakili Halima Sonda

Naye Mkurugenzi wa Mkurugenzi  wa Miradi na Uendeshaji wa (THRDC), Wakili Halima Sonda akizungumzia Ukatili dhidi ya waandishi wa habari wanawake, alitaka wanahabari wanawake wapewe fursa sawa na waume katika kuandika habari za uchunguzi za mazingira.

Hata hivyo, alisema kumekuwepo udhalilishaji wa wanawake mitandaoni, mifumo dume katika jamii mambo ambayo yanapaswa kupingwa kwani tayari kuna sheria kadhaa, zinazopinga ukatili dhidi ya wanawake na wanahabari wanawake wa mazingira wanapaswa kuzijua.

Mafunzo hayo kwa waandishi kanda ya Kati, kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Iringa, Morogoro ni mfululizo wa mafunzo yanayotolewa na THRDC na MAIPAC kwa wanahabari nchini kupitia mradi wa  kuwezesha waandishi wa habari za mazingira kuimarisha uwezo wa wanahabari ili kuchangia uwajibikaji  wa mazingira na kukuza uelewa katika jamii tayari mafunzo yametolewa kanda ya kaskazini na Kanda ya Ziwa.







MWISHO

No comments: