DEREVA BAJAJI ASHIKILIWA KWA KUJERUHI NA KUSABABISHA KIFO CHA BAJAJI MWENZAKE MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 16 September 2026

DEREVA BAJAJI ASHIKILIWA KWA KUJERUHI NA KUSABABISHA KIFO CHA BAJAJI MWENZAKE MOROGORO

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo

Na Lilian Kasenene, Morogoro 

maipacarusha20@gmail.com 


KIJANA Joshua Wilfred Lukoo(25) maarufu kwa jina la Kideni mkazi wa Mazimbu Ipoipo anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumjeruhi na kusababisha kifo cha dereva mwenzake wa bajaji, Cyprian Augustino maarufu Sembe(26) mkazi wa Mazimbu.


Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, imeeleza tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 12, 2026, katika eneo la Ipoipo, Kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro.


Taarifa hiyo inaeleza kuwa tukio hilo lilitokana na ugomvi uliosababishwa na suala la malipo ya kazi ya bajaji.


Inadaiwa kuwa mtuhumiwa Joshua Wilfred Lukoo alimkabidhi marehemu bajaji yenye namba za usajili MC 665 FJM kwa ajili ya kufanya kazi. 


Baada ya kumaliza kazi, marehemu alirejesha bajaji hiyo pamoja na kiasi cha Shilingi 20,000 kwa mtuhumiwa lakini mtuhumiwa hakuridhika na kiasi hicho, hali iliyosababisha kutokea kwa ugomvi kati yao.


Katika purukushani hiyo, mtuhumiwa anadaiwa kumjeruhi marehemu kwa kutumia kitu chenye makali, ambapo alichomwa katika eneo la kifua upande wa kushoto.


Baada ya kujeruhiwa, Cyprian alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu hata hivyo, kutokana na hali yake kuwa mbaya, alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ambako baadaye alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku likitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano na taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi wa matukio ya aina hiyo.


Aidha, Jeshi la Polisi limewasisitiza wananchi kuepuka kutumia nguvu au silaha katika kutatua migogoro, badala yake kutumia njia za amani na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapokumbana na migogoro.


Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Septemba 16,2026.


........

No comments: