Na SEIF TAKAZA IRAMBA
maipacarusha20@gmail.comWAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemtaka Mkandarasi anaetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika katika kitongoji cha Igumo Wilayani Iramba Mkoa wa Singida amalize mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Waziri Aweso amesema, Mkandarasi huyo anapaswa kutekeleza mradi huo kwa sababu fedha za ukamilishaji wa mradi huo zipo "Kuanzia sasa nakuagiza ufanye kazi usiku na mchana ili kuongeza nguvu ya ukamilishaji wa mradi huu hivyo ifikapo Mwezi Machi mwakani wananchi wa mji wa Kiomboi waweza kupata maji ya uhakika" aliagiza Aweso
Hata hivyo, mahitaji ya maji katika Mji wa Kiomboi ni lita milioni 3, ambapo kwa Sasa Mamlaka ya maji Kiomboi inazalisha maji lita Milioni moja tu hivyo upungufu wa maji ni zaidi ya lita milioni 2, ndiyo maana Mbunge wa Jimbo hili na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameona haja ya kumuomba Mhe. Rais kujenga mradi mkubwa wa maji, ili kumaliza kabisa tatizo la maji.
"Aidha sisi tumekubaliana na uongozi wa Wilaya kuongeza kisima kingine cha tano ambapo hapo awali ilikua kuchimba visima vinne tu" Alisema
Akimkaribisha Waziri Aweso Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Alhaji Suleiman Mwenda, amesema suala la maji katika mji wa Kiomboi, limekuwa hoja ya msingi kwani kwa muda mrefu, maji hayajatosheleza hivyo mradi huu utasaidia kukidhi mahitaji ambayo yatakidhi mahitaji ya mji ambapo kwa sasa maji yanatoka kwa muda mfupi na kwa siku maalum.
Kwa mujibu wa taarifa ya Utekelezaji wa mradi iliyoandaliwa na KIUWASA kuwa Mradi wa Maji wa miji 28 ni miongoni mwa miradi unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( KIUWASA) ambao unajengwa na Kampuni ya Megha Engineering and Infrastrures Ltd kuoka India na Mhandisi Mshauri WapcosLtd kutoka India.
Taarfa hiyo Inaeleza kuwa Mradi huo ulisainiwa Juni 06 2022 na ulitarajiwa kukamilika Agosti 10 2026 lakini kutokana na changamoto mbalmbali Mkandarasi ameomba kukamilisha ifikapo mwezi Julai 2027.
Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 15 ambao utawanufaisha wananchi 44,487 wa Mji wa Kiomboi ambao hadi sasa upo asilimia 10.
Katika mradi huo changamoto zilizojitokeza ni pamoja na kukosekana kwa maji chini ya ardhi ambapo hapo awali Mkandarasi alichimba visima maeneo ya Meli, Magula ,Ruruma na Tutu ambapo kisima kimoja tu eneo la Meli kilipatikana lita 12000 kwa sasa. Hata hivyo Mkandarasi alifanya utafiti eneo la Ulemo na kuweza kuchimba visima vitatu vyenye uwezo wa kutoa lita 38000,lita 21000 na lita 20000.
Akitoa Shukrani kwa Waziri, Diwani wa Kata ya Kiomboi Omary Hassan Omary, amemuomba Waziri kwa namna itakavyo mpendeza aweze kuisaidia Mamlaka ya maji Kiomboi, ili iweze kujitegemea na kuwafikia Wananchi kwa utoaji wa huduma Bora.
Akitoa Shukrani kwa Waziri, Diwani wa Kata ya Kiomboi Omary Hassan Omary, amemuomba Waziri kwa namna itakavyo mpendeza aweze kuisaidia Mamlaka ya maji Kiomboi, ili iweze kujitegemea na kuwafikia Wananchi kwa utoaji wa huduma Bora.
Kwa upande wake mama mmoja wa kitongoji cha Igumo Elizabeth Kitila amesema amefarijika sana kumuona Waziri wa maji na kumuomba apeleke salamu za Shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kumtua mama ndoo kichwani
Waziri Aweso alikua akikagua tenki la maji linalojengwa katika kitongoji cha Igumo nje kidogo mwa mji wa Kiomboi.
MWISHO


No comments:
Post a Comment