MWIGULU: VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI VIMEPUNGUA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 80 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 9 September 2026

MWIGULU: VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI VIMEPUNGUA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 80

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba



 


Na Mwandishi wetu,Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amesema vifo vitokanavyo na uzazi duniani vimepungua kwa kiwango kikubwa, huku akieleza kuwa Tanzania imeendelea kupiga hatua katika kuboresha huduma za afya ya msingi.



Mwigulu ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Afya ya Msingi 2026, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan


Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi, ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati.


“Mkutano huu utoe fursa ya tafakari kwa pamoja kama nchi, bara na hata ulimwengu, kwani Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwenye sekta ya afya ngazi ya msingi,” amesema Mwigulu.

Amesema suala la rasilimali fedha linapaswa kupewa kipaumbele ili kuwezesha nchi kufikia viashiria endelevu katika sekta ya afya.


Aidha, Waziri Mkuu amesema Tanzania na nchi nyingine bado zina changamoto katika kupokea na kutumia tafiti za kisayansi kwa kiwango kinachohitajika, huku akieleza kuwa Tanzania tayari imeanza kuchukua hatua katika eneo hilo.


Mwigulu amesema Serikali pia inalenga kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini ili kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje.


“Dira ya Serikali ya Tanzania sasa inahama kutoka kwenye kupokea dawa nje ya nchi na badala yake viwanda viwekezwe viwe vingi ili kuepusha changamoto mbalimbali,” amesema.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetoa ajira mpya kwa wataalamu wa sekta ya afya, huku katika kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 ikipanga kujenga zaidi ya nyumba 2,000 kwa ajili ya watumishi wa afya.

Mkutano huo umewakutanisha zaidi ya wadau 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi na mifumo endelevu ya kugharamia huduma hizo.

Naye Profesa Riziki Shemdoe amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika huduma za afya ya msingi, akieleza kuwa takwimu zinaonesha wajawazito milioni 2.9, sawa na asilimia 95, wameweza kujifungulia katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amosi Makalla, amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya mkoani humo kupitia ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya pamoja na upatikanaji wa magari ya wagonjwa.

Amesema Serikali imetoa kiasi cha Sh bilioni 94 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya mkoani Arusha.


Kauli mbiu ya mkutano huo ni kuelekea Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Wote kwa Kuimarisha Mifumo Endelevu ya Kugharamia Huduma za Afya, Kuongeza Ufanisi na Kuboresha Ubora wa Huduma Ndani ya Huduma za Afya ya Msingi.”

No comments: