![]() |
| Mwakilishi wa Africa Tourism Partners, Devotha Mdachi |
Na Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Mawakala wa utalii kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali ya Afrika wanatarajiwa kukutana Jijini Arusha kupitia ziara ya utangazaji wa utalii itakayoanza Septemba 27, 2026 Zanzibar na kuendelea Arusha, ikiwa na lengo la kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo na kufungua fursa mpya za masoko katika sekta ya utalii.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Mwakilishi wa Africa Tourism Partners, Devotha Mdachi, amesema ziara hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Africa Tourism Private Sector Alliance itatoa fursa kwa mawakala wa utalii kukutana, kujenga mahusiano ya kikazi na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuendeleza na kutangaza utalii barani Afrika.
Amesema ziara hiyo itaanzia Zanzibar Septemba 27, na baadae kuelekea Jijini Arusha, ambako mawakala watapata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya utalii.
Mdachi amesema moja ya changamoto kubwa inayowakabili mawakala wa utalii kwa sasa ni upatikanaji wa masoko makubwa, hivyo ziara hiyo inalenga kuwasaidia wadau kujenga mitandao mipya ambayo inaweza kufungua fursa za kibiashara.
Amesema kupitia mikutano hiyo, mawakala wataweza kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa shughuli za utalii, jambo litakalosaidia kuongeza ushirikiano baina ya wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Aidha, amesema ziara hiyo itatoa fursa kwa washiriki kufahamu fursa mbalimbali za utalii zilizopo nchini Tanzania, ikiwemo zile zinazohusiana na michezo ya Africon.
Katika hatua nyingine alisema kuwa mawakala wa utalii wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa masoko lakini pia panapotokea ziara kama hizo za utangazaji wa fursa za utalii wanatakiwa kushiriki na kubadilishana uzoefu
"Mawakala kutoka maeneo mbalimbali watakuwepo kwenye ziara hiyo lakini pia tutahakikisha kuwa watabadilishana uzoefu hii itasaidia sana kupanua soko la mazao ya utalii "aliongeza
Ametoa wito kwa mawakala wa utalii, hususan waliopo Jijini Arusha, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara hiyo ili kutumia fursa hiyo kujenga mahusiano mapya ya kikazi, kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko mapya ya utalii.

No comments:
Post a Comment