Na Mwandishi wetu, Nzega
maipacarusha20@gmail.com
HALMASHAURI ya Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, imesajili vikundi 203 vikijumuisha wazee 11, wanawake 108, vijana 79 na watu wenye ulemavu watano.
Afisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, AnnaMary Galibona ameeleza hayo mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang'onda akisoma taarifa ya usajili na ushiriki wa makundi maalumu kwenye mfumo wa ununuzi wa umma (PPRA).
Galibona ameeleza kwamba hadi kufikia Septemba mwaka 2026 vikundi hivyo vimeshasajiliwa na Halmashauri hiyo na wana mikakati ya kuongeza zabuni kwa makundi maalum.
Amesema kwa mwaka 2026 vikundi tisa vimetunukiwa zabuni mbalimbali zenye thamani ya shilingi 76,000,000 ambapo vikundi viwili vipo katika hatua ya utekelezaji wa mikataba ya thamani ya shilingi 13,000,000 na vikundi saba vipo hatua ya kusaini mikataba yenye thamani ya 63,000,000 iliyotolewa na TARURA.
Amesema hiyo ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 inayoeleza kila taasisi za umma kutumia asilimia 30 ya bajeti yake ya manunuzi kwa mwaka kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
"Halmashauri kupitia bajeti ya mwaka 2026/27 imepanga kufanya manunuzi ya shilingi 6,134,650,506 ambapo shilingi 1,840,395,152,80. sawa na asilimia 30 ya bajeti tajwa itatumika kwenye zabuni ya makundi maalumu," amesema Galibona.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Lemea Tukai ametoa shukrani za dhati kwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya makundi maalum.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia kwa kujali makundi haya hususan vijana ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo," amesema DC Tukai.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang'onda ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa kujali makundi hayo maalum.
"Hongera sana Mheshimiwa DC kwa kumheshimisha Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani halmashauri ya Nzega DC imevuka malengo katika usajili," amesema Mwang'onda.
MWISHO

No comments:
Post a Comment