VYUO VYAJADILI UENDELEVU NA UBORA WA ELIMU YA JUU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 6 September 2026

VYUO VYAJADILI UENDELEVU NA UBORA WA ELIMU YA JUU

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

Mwandishi Wetu, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Viongozi wa vyuo vikuu nchini wamekutana kujadili uendelevu na namna ya kuimarisha ubora wa elimu ya juu, pamoja na kujiandaa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi, mahitaji ya soko la ajira na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.


Kikao hicho kilichofanyika Septemba 5, 2026 jijini Dodoma, kimewakutanisha Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu, Makamu Wakuu wa Vyuo na viongozi wengine wa taasisi za elimu ya juu, kwa lengo la kujadili kwa pamoja namna ya kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa vyuo na kuhakikisha elimu inayotolewa inaendelea kuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya Taifa.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni namna ya kuhakikisha vyuo vinakuwa na uwezo wa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi bila kuathiri ubora wa elimu, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia uwezo wa taasisi katika kutoa huduma bora za elimu.


Amesema suala la udahili wa wanafunzi ni sehemu ya mjadala huo, ambapo taratibu zinapaswa kuendelea kuzingatia uwezo wa vyuo, miundombinu, rasilimali watu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ili ongezeko la wanafunzi liende sambamba na uhakika wa ubora wa elimu.


Aidha, amesema Serikali inaendelea kupanua fursa za elimu ya juu kupitia uwekezaji katika miundombinu na kampasi mpya katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu na kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za masomo.


Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, amesema kikao hicho kimekuwa fursa muhimu kwa viongozi wa vyuo vikuu kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazolikabili eneo la elimu ya juu, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na mabadiliko na mahitaji ya sekta hiyo.


Prof. Kihampa amesema ongezeko la wanafunzi linalotarajiwa kutokana na utekelezaji wa sera  linahitaji maandalizi ya pamoja, akisisitiza kuwa upanuzi wa fursa za elimu ya juu unapaswa kwenda sambamba na kulinda na kuimarisha ubora wa elimu.

No comments: