Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Miili 29 imepatikana na majeruhi 30 wameokolewa katika ajali mbaya iliyohusisha basi la abiria la Dream Line na lori lililokuwa limebeba miti aina ya mirunda, katika eneo la Mkambarani, Kikombe cha Chai, barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam, mkoani Morogoro.
Mamlaka zinaendelea na uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa Oktoba 8, mwaka huu.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 902 ENG na basi lenye namba T 672 ELT, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya. Magari hayo yaligongana uso kwa uso, huku basi likiteketea kwa moto na kufanya zoezi la uokoaji kuwa gumu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kujaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari katika eneo lisiloruhusiwa.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, amesema kikosi chake kiliongeza magari ya uokoaji baada ya kubaini ukubwa wa ajali na moto uliokuwa umesambaa.
Mwasabeja amesema kipaumbele cha kwanza kilikuwa kuokoa maisha ya watu. Ameeleza kuwa kikosi chake kilifanikiwa kutoa miili 29 na kusaidia majeruhi 30 kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Ameongeza kuwa idadi rasmi ya vifo na majeruhi inapaswa kuthibitishwa na wataalamu wa afya.
Miongoni mwa manusura ni Obtato Mwanyigu, ambaye amesema alishuhudia lori likihama kutoka upande wake wa barabara na kuelekea upande ambao basi walimokuwa wakisafiria lilikuwa likipita.
Abiria wengine wamesema ajali hiyo ilikuwa mbaya sana na kutoa wito kwa madereva kuzingatia tahadhari na sheria za barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha.
Katika tukio jingine, Polisi imethibitisha kutokea kwa ajali eneo la Miti Bora, kati ya Dakawa na Dumila, wilayani Mvomero. Ajali hiyo ilihusisha gari la Polisi lililokuwa na askari waliokuwa kazini na lori aina ya Scania linalomilikiwa na kampuni ya ATT.
Kantimbo amesema watu wanne walifariki katika ajali hiyo, huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Wakati uchunguzi ukiendelea, mamlaka husika zinatarajiwa kutoa taarifa zaidi zitakazobainisha idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali ya Mkambarani pamoja na utambulisho wa waathirika.
.....





No comments:
Post a Comment