BAADA YA MGOGORO WA MUDA MREFU SASA JAMII YA MAASAI YAPEWA HATI MILIKI YA ENEO LA MILA LA ELERAI LENYE EKARI 23 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 17 October 2026

BAADA YA MGOGORO WA MUDA MREFU SASA JAMII YA MAASAI YAPEWA HATI MILIKI YA ENEO LA MILA LA ELERAI LENYE EKARI 23

  



Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira

mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


Jamii ya Maasai imepokea hati miliki ya eneo la Elerai lenye ukubwa wa ekari 23, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baada ya mgogoro wa muda mrefu kuhusu umiliki wa eneo hilo lililopo katika eneo la Burka Estate, Arusha.


Makubaliano hayo yamefikiwa kupitia utiaji saini kati ya viongozi wa jamii ya Maasai kupitia Baraza la Marya na wakurugenzi wa Burka Estate, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, iliyowakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.


Jamii ya wamasai wakishuhudia utiaji wa saini 

Kupitia makubaliano hayo, eneo hilo litatumika kwa shughuli za mila na utamaduni wa jamii ya Maasai, kwa mujibu wa masharti yaliyokubaliwa na pande husika, likiwa na umuhimu mkubwa katika kuhifadhi urithi wa jamii hiyo.


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameitaka jamii ya Maasai kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na kuhakikisha eneo hilo linatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, hususan kuendeleza na kuhifadhi mila na utamaduni wao.


Makabidhiano hayo yanaashiria hatua muhimu katika juhudi za kumaliza mgogoro wa umiliki wa eneo hilo na kuhakikisha jamii ya Maasai inaendelea kuhifadhi urithi wake wa mila na utamaduni kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments: