Mwandishi Maalumu RS Arusha
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila, ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Mkoa wa Arusha kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, huku akisisitiza kuimarishwa kwa tahadhari na utoaji wa elimu ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini kupitia mpaka wa Namanga unaounganisha Tanzania na Kenya.
Dkt. Nguvila ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, wakati akikagua maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo katika Kituo cha huduma za pamoja Namanga, Wilaya ya Longido, akiwa ameambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido.
Amesema Mkoa wa Arusha umeshatoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ya 100 kuhusu utayari na namna ya kukabiliana na Ebola, huku Serikali kupitia Wizara ya Afya ikiwa imeleta vifaa vya awali vitakavyotumika endapo ugonjwa huo utaingia nchini. Aidha, halmashauri zote saba za mkoa zimetenga vituo kwa ajili ya kuwatunza na kuwahudumia wale wote watakaobainika kuwa na maambukizi.
Dkt. Nguvila amesisitiza kuwa watumishi wa kituo cha Namanga wanapaswa kuwachunguza kwa umakini wasafiri wanaoingia nchini, ikiwemo kupima joto la mwili na kuwafanyia uchunguzi zaidi wale watakaokuwa na viashiria vya ugonjwa huo, akieleza kuwa kudhibiti maambukizi mpakani kutasaidia kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo maeneo mengine.
Aidha, amewataka wataalamu na wananchi kuongeza umakini, kuzingatia maelekezo ya kiafya na kutoa elimu kwa jamii kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa, ikiwemo kuepuka mazoea ya kushikana mikono na kukumbatiana katika mazingira yanayohitaji tahadhari, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha Ebola haiingii nchini na kulinda maisha ya wananchi.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment