![]() |
Na Mwandishi wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Arusha. Shirika la DSW Tanzania kupitia Mradi wa REST linashirikiana na mashirika 11 yasiyo ya kiserikali kutoa elimu ya afya ya uzazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana katika mikoa sita nchini.
Mradi huo unalenga kuongeza uelewa wa vijana wa kike na wa kiume kuhusu afya ya uzazi, kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuwawezesha kufikia malengo yao ya maisha.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya mradi huo kilichofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi wa DSW Tanzania na mshauri wa uendeshaji wa mashirika, Peter Owaga, amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa taasisi zinazohudumia vijana ili ziweze kutoa huduma bora na endelevu katika jamii.
Amesema vijana wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi, hali inayoweza kuwaathiri katika kufanya maamuzi yanayohusu afya na mustakabali wa maisha yao.
Owaga amesema pamoja na kutoa elimu, mradi huo unaunganisha wadau wa huduma za vijana na kuwajengea uwezo wa kushirikiana kutatua changamoto zinazowakabili vijana, huku wakiwezeshwa kutumia fursa zilizopo kuboresha maisha yao.
“Hatujajenga uwezo wa taasisi kwa kuangalia mifumo yake pekee, bali pia namna inavyoweza kuleta mabadiliko katika jamii. Tunataka taasisi ziwe na uwezo wa kuendelea kuwahudumia vijana hata pale mradi unapomalizika,” amesema.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya mashirika, wataalamu wa Serikali, viongozi wa dini, watoa huduma za afya na vijana wenyewe ni muhimu katika kuhakikisha elimu na huduma zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya jamii.
Vijana 600 wafikiwa Chunya
Akizungumzia matokeo ya mradi huo katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, mdau wa mradi huo, Mariam Mintanga, amesema takribani vijana 600 wamefikiwa kwa elimu ya afya ya uzazi na mbinu bunifu za maisha.
Amesema eneo hilo linakabiliwa na changamoto zinazohusishwa na shughuli za uchimbaji wa madini, ambazo baadhi ya vijana huanza kushiriki wakiwa na umri mdogo, hali inayoweza kuchangia kuacha shule na kuingia katika mahusiano ya kingono mapema.
“Tumetumia mradi huu kuwajengea vijana uelewa kuhusu afya ya uzazi na umuhimu wa kubaki shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao. Pia tumewahamasisha kutafuta taarifa sahihi na kutumia huduma rafiki za afya zinazopatikana katika maeneo yao,” amesema.
Mintanga amesema bado baadhi ya vijana wanakosa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi, wakiwemo wanaotumia dawa kwa kufuata ushauri wa wenzao bila kupata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Amesema wengine wanaokabiliwa na magonjwa ya zinaa hawafiki katika vituo vya afya kupata uchunguzi na matibabu, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuimarisha upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana.
Ukeketaji wapungua Monduli
Katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Shirika la Voyota limesema juhudi za kutoa elimu kupitia mradi huo zimechangia mapambano dhidi ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia, hususan katika jamii za wafugaji.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, mwakilishi wa shirika hilo, Lilian Munguri, amesema takwimu za Voyota zinaonyesha kiwango cha ukeketaji katika eneo wanakofanyia kazi kimepungua kutoka asilimia 49 hadi asilimia 44.
“Tumefanya kazi na vinara wa vijana na viongozi wa jamii kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji. Jambo la kutia moyo ni kuona wazee wa mila wakitambua kuwa ukeketaji ni changamoto na kuanza kushiriki katika juhudi za kuachana na mila hiyo,” amesema.
Munguri amesema ushiriki wa viongozi wa jamii na wazee wa mila ni muhimu katika kuhamasisha mabadiliko ya mitazamo na kuimarisha juhudi za kukomesha vitendo vinavyohatarisha afya na ustawi wa wasichana.
DSW yataka huduma rafiki kuimarishwa
Naye Shamsa Halfan kutoka DSW Tanzania amesema Mradi wa REST unatekelezwa katika mikoa sita kupitia mashirika 11, ukiweka mkazo katika kuwawezesha vijana kupata taarifa na huduma za afya ya uzazi zinazokidhi mahitaji yao.
Amesema pamoja na kuimarisha huduma hizo, ni muhimu kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wake na kuondoa hofu na vikwazo vinavyoweza kuwazuia vijana kuzitumia.
Amesisitiza kuwa vituo vya afya vinapaswa kuendelea kuboresha huduma ili vijana wanapovitembelea wapate taarifa sahihi, ushauri na matibabu yanayokidhi mahitaji yao.
Serikali yasema ushirikiano ni muhimu
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Malezi na Familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Imelda Kamugisha, amesema juhudi hizo zinaunga mkono ajenda ya Taifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo ya vijana balehe iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia Februari 2021 hadi Juni 2025.
Amesema utekelezaji wa ajenda hiyo ulihusisha wizara za kisekta, taasisi za Serikali, mashirika ya kiraia, taasisi za dini, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha programu zinazolenga vijana zinaendana na sera na miongozo ya Taifa.
“Afya na maendeleo ya vijana balehe si jukumu la sekta moja pekee. Tunahitaji shule, taasisi za dini, viongozi wa jamii, sekta ya afya na washirika wa maendeleo kufanya kazi kwa pamoja ili kuwajengea vijana mazingira yanayowawezesha kufanya maamuzi sahihi na kutimiza ndoto zao,” amesema.
Kamugisha amesema Serikali inaendelea kutambua mchango wa mashirika ya kiraia katika kuimarisha upatikanaji wa taarifa na huduma za afya ya uzazi, kujenga uwezo wa taasisi za ndani na kuongeza ushiriki wa vijana katika masuala yanayowahusu.
Mwisho




No comments:
Post a Comment