ESAP YARAHISISHA SOKO LA VILIPUZI MIGODINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 2 October 2026

ESAP YARAHISISHA SOKO LA VILIPUZI MIGODINI

 


Na Mwandishi wetu, Geita


maipacarusha20@gmail.com 


KAMPUNI ya kizawa ya Tanzania inayojihusisha na usambazaji wa vilipuzi na huduma za ulipuaji katika sekta ya madini ( ESAP) imesema kuwa  imewekeza katika teknolojia na mitambo ya kisasa ili kuongeza uwezo wa kuhudumia migodi mikubwa, ya kati na wachimbaji wadogo nchini


Mkurugenzi wa kampuni ya ESAP Yahya Puyaga ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan manispaa ya Geita.


Puyaga amesema kuwa  uwekezaji huo umewezesha kampuni kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini na kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya migodi nchini.


Amesema tofauti na kampuni nyingi zinazofanya biashara ya usambazaji wa vilipuzi katika Afrika Mashariki ambazo zinatoka nje ya nchi, kampuni hiyo ni ya kizawa na inamilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.


“Local content imetuwezesha sisi kuweza kufika na kutoa huduma katika sehemu mbalimbali. Tumewekeza katika teknolojia ya kisasa na mitambo inayotuwezesha kutoa huduma kulingana na mahitaji ya sekta ya madini,” alisema Puyaga.


Amesema kampuni  hiyo kwa sasa inasambaza vilipuzi katika baadhi ya migodi nchini, ikiwemo Bulyanhulu, STAMIGOLD na Shanta, huku pia ikitoa huduma za ulipuaji katika maeneo mengine ya migodi.


Kwa upande wa uzalishaji amesema kampuni imewekeza katika kiwanda kilichopo Wilaya ya Bukombe, kinachosaidia kuongeza uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji.


Hata hivyo  amesema kampuni imeagiza magari maalumu yanayoweza kuchanganya vilipuzi katika maeneo ya migodi, ambapo baadhi ya magari hayo yanafanya kazi katika maeneo mbalimbali ili kuongeza ufanisi na usalama wa huduma.


Amesema kupitia uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya local content, kwa kuwa unawawezesha Watanzania kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma zinazohusiana na sekta ya madini.


"Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata vifaa na bidhaa zinazokidhi mahitaji yao, hasa kwa kuwa wengi wao wanafanya uchimbaji wa chini ya ardhi (underground mining)," amesema.


Amesema bidhaa hizo zitakapopatikana kwa kiwango kinachohitajika, zitawasaidia wachimbaji wadogo kupata huduma na vifaa kwa gharama nafuu zaidi huku zikiendelea kuzingatia teknolojia na viwango vinavyotakiwa katika sekta ya madini.


Baadhi ya wadau wa madini Geita wameipongeza kampuni ya ESAP kwa namna inavyotoa huduma kwenye sekta ya madini.


MWISHO

No comments: