![]() |
Lilian Kasenene, Morogoro
Maipacarusha20@gmail.com
MASHINDANO ya mbio za magari ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yamezinduliwa rasmi mkoani Morogoro, huku magari zaidi ya 24 yakitarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho katika viwanja vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), eneo la Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.
Uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika katika Kiwanda cha Serengeti na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mussa Kilakala, ambaye amewataka washiriki na watazamaji kuzingatia usalama wakati wote wa mashindano.
![]() |
Kilakala pia amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, akiwataka washiriki, mashabiki na wananchi wanaokwenda kushuhudia mashindano hayo kuhakikisha shughuli zao haziathiri uoto wa asili na mazingira ya Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Uzalishaji Mbegu za Miti, Dk. Hamza Kateti, amesema TFS itaendelea kusimamia na kulinda mazingira katika maeneo ya misitu, ambayo ni muhimu kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
![]() |
Dk. Kateti amewahimiza wananchi kutumia fursa ya mashindano hayo kujifunza kuhusu uhifadhi na kufanya utalii wa ikolojia kwa kutembelea hifadhi na maeneo mbalimbali ya asili yanayopatikana mkoani Morogoro na yanayosimamiwa na TFS.
Kwa upande wa madereva, wameeleza kuridhishwa na hali ya njia iliyotumika katika maandalizi ya mashindano hayo, wakisema ina changamoto zinazohitajika katika mbio za magari na hivyo kutoa nafasi ya ushindani.
Dereva Kartik Valambia, anayeshiriki katika mashindano hayo, amesema njia hiyo imewaandaa vizuri madereva na kutoa fursa ya kuonyesha uwezo wao wa kuendesha magari katika mazingira yenye changamoto.
Naye dereva Tufail Amin amesema ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa kutokana na ubora na changamoto za njia, huku kila dereva akiingia kwenye mashindano akiwa na mkakati wa kufanya vizuri.
Mashindano hayo yanashirikisha zaidi ya magari 24, ambapo magari tisa yanashiriki katika African Rally Championship (ARC).
Timu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na India zinashiriki katika mashindano hayo yanayofanyika katika maeneo ya TFS mkoani Morogoro.
Magari hayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho , huku mashabiki wakitarajia kushuhudia ushindani mkubwa katika njia zenye changamoto za Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.
....





No comments:
Post a Comment