![]() |
| Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba |
![]() |
Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba, amewataka wataalamu wa chuo hicho kubuni njia mbalimbali za kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kufanya shughuli zao kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa ili kujikwamua katika umaskini na kukuza uchumi.
Jaji Warioba aliyasema hayo baada ya kuwatunuku wahitimu wa SUA katika ngazi mbalimbali wakati akizungumza kwenye Mahafali ya 48 ya chuo hicho.
Alieleza kuwa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuinua maisha ya Watanzania, umaskini bado ni changamoto kubwa, hususan kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Alisema baada ya Uhuru, Serikali ilitangaza maadui watatu wa maendeleo ambao ni maradhi, ujinga na umaskini, na kwamba katika kukabiliana na maradhi na ujinga hatua kubwa zimepigwa kupitia ujenzi wa hospitali na upanuzi wa fursa za elimu, huku changamoto kubwa iliyosalia ikiwa ni kupambana na umaskini.
![]() |
| Wahitimu |
“Baada ya Uhuru ilitangazwa maadui watatu ambao ni maradhi, ujinga na umasikini, ila kwenye elimu Serikali imejitahidi, shule zipo kila kona ya nchi na kwenye afya hospitali zimejengwa kila kata. Changamoto imebaki kupambana na umasikini,” alisema Jaji Warioba.
Alisema SUA ina nafasi ya pekee katika kupambana na umaskini kwa kuwawezesha wakulima kuachana na kilimo cha kujikimu na badala yake kufanya kilimo biashara kinachowawezesha kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, wakulima wengi wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika uzalishaji lakini mwisho wa siku hawapati faida inayolingana na uwekezaji wao, huku wafanyabiashara wanaonunua mazao kwa bei ndogo wakiwa miongoni mwa wanaonufaika zaidi kwa kuyauza kwa bei ya juu.
Alisema Serikali inapaswa pia kuendelea kuwawezesha wakulima kwa kutoa ruzuku katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa uzalishaji na kuwapatia zana za kisasa za kilimo, badala ya kuwekeza zaidi katika ruzuku ya mbolea pekee.
*BARAZA LA SUA LAHIMIZA MATUMIZI YA TAFITI KUTATUA CHANGAMOTO ZA JAMII*
Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Andrew Massawe, amesema Baraza linaendelea kusimamia matumizi ya matokeo ya tafiti zinazofanywa na chuo hicho katika kuboresha sera, mipango na mikakati ya maendeleo, kwa lengo la kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
![]() |
| Makamu mkuu wa chuo kikuu SUA, Prof chibunda |
Massawe alisema utafiti na ubunifu umepewa nafasi muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya SUA, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuai.
Alisema Baraza limeidhinisha kuanzishwa kwa Taasisi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Bioanuai (Climate Change and Biodiversity Institute), ambayo inalenga kuimarisha tafiti na ubunifu katika kutafuta suluhisho la changamoto za kimazingira.
Aidha, alisema Baraza limeendelea kufuatilia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Sita wa SUA wa mwaka 2026–2031 wenye malengo tisa ya kimkakati.
Kwa mujibu wa Massawe, katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, SUA imefanikiwa kutekeleza shabaha zilizopangwa kwa wastani wa asilimia 80, huku Sh bilioni 125.77 zikitumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.
Alisema Baraza pia linaendelea kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya Sh bilioni 62.78, unaolenga kuboresha miundombinu ya elimu katika kampasi mbalimbali za SUA.
Kupitia mradi huo, alisema chuo kinajenga majengo manane katika Kampasi za Mizengo Pinda, Edward Moringe na Solomon Mahlangu.
Majengo hayo yanajumuisha mabweni mawili, kumbi tatu za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kila moja, jengo mtambuka la Ndaki ya Biashara na Uchumi pamoja na maabara za mafunzo kwa vitendo.
Massawe amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa mujibu wa muda uliowekwa katika mikataba.
Katika kuimarisha utendaji wa chuo, Baraza limeidhinisha Mpango Mkakati wa Sita wa SUA wa mwaka 2026–2031 pamoja na sera mbalimbali, zikiwemo Sera ya Usalama wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Sera ya Elimu Mtandao, Sera ya Usimamizi wa Kumbukumbu za Chuo na Sera ya Utoaji Huduma na Ushirikishwaji wa Jamii, zote za mwaka 2026.
Kwa upande wa rasilimali watu, Massawe alisema Baraza limewapandisha vyeo wanataaluma sita kuwa Maprofesa na wanataaluma 14 kuwa Maprofesa Washiriki, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa chuo katika ufundishaji, utafiti na huduma kwa jamii.
Alisema pia Baraza limeendelea kusimamia maboresho ya mitaala ili kuhakikisha programu zinazotolewa na SUA zinaendana na mahitaji ya soko la ajira, maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na mahitaji ya sekta za uzalishaji.
Alisema maboresho hayo yamejikita pia katika kuimarisha mafunzo ya vitendo kupitia mashamba darasa, karakana na maabara, huku wataalamu kutoka sekta husika wakishirikishwa katika ufundishaji.
Kwa utaratibu huo, asilimia 20 ya mafunzo itatolewa na wataalamu kutoka sekta za uzalishaji na viwanda, kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mazingira halisi ya kazi.
Massawe alisema mapitio ya mitaala yamekamilika na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetoa ithibati na kuruhusu SUA kuanza kutumia mitaala mipya 111 ya kimkakati katika mwaka wa masomo 2026/2027.
Aidha, alisema Baraza limeendelea kusimamia mapato na matumizi ya fedha za chuo kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na nidhamu ya kifedha, huku mifumo ya udhibiti wa ndani ikiimarishwa ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi.
Alisema juhudi pia zinaendelea katika kuongeza mapato ya ndani kupitia miradi ya kibiashara, huduma za ushauri wa kitaalamu na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati.
*WAHITIMU 3,309 WATUNUKIWA VYETI*
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 3,309 wametunukiwa vyeti kutoka programu 69 za masomo, huku wanawake wakiwa 1,535, sawa na asilimia 46.39 ya wahitimu wote.
Akizungumza katika sherehe hizo, Makamu wa Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, alisema kati ya wahitimu hao, 3,156 ni wa Shahada za Kwanza, 62 Shahada za Umahiri, 22 Shahada za Uzamivu, wanne Stashahada ya Uzamili, 60 Stashahada na watano Astashahada.
Profesa Chibunda alisema SUA imeendelea kupata mafanikio mbalimbali, ikiwemo kuanzisha programu mpya tano za masomo zilizoidhinishwa na TCU kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Alisema chuo pia kinaendelea kutekeleza miradi 116 ya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini, huku zaidi ya watumishi 226 wakiwa katika mafunzo ya umahiri na uzamivu ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema SUA imeanza shughuli za Kampuni ya Uzalishaji Mapato na Huduma za Chuo kwa lengo la kuongeza vyanzo vya mapato na kuimarisha uwezo wa chuo kujitegemea kifedha.
Profesa Chibunda pia alisema chuo kimepata idhini ya Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kuendesha programu ya kikanda ya Shahada ya Umahiri ya Sayansi katika Uhandisi na Usimamizi wa Umwagiliaji.
*WAHITIMU WAWE WABUNIFU NA WAANDAAJI WA AJIRA*
Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Andrew Massawe, aliwataka wahitimu kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni kubadilisha changamoto kuwa fursa, kuwa wabunifu na waandaaji wa ajira badala ya kuwa watafuta ajira pekee.
Amesema wahitimu wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika sekta za kilimo, ufugaji, teknolojia na ujasiriamali ili kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine.
“Thamani ya elimu yenu haitapimwa kwa cheti mtakachopokea leo, bali kwa matokeo mtakayoyaacha katika maisha ya watu na maendeleo ya Taifa,” alisema.
Massawe aliwataka pia wahitimu kuendelea kujifunza na kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kazi, akisisitiza kuwa kuhitimu si mwisho wa kujifunza.
Aliwapongeza wahitimu hao kwa kufikia hatua hiyo muhimu, huku akiwashukuru wanataaluma, wafanyakazi, wazazi na walezi kwa mchango wao katika kuwawezesha wanafunzi kukamilisha masomo yao.
Mahafali ya 48 ya SUA yamefanyika leo, Oktoba 8, 2026, yakishirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, mabalozi, wadau wa kitaifa na kimataifa, wanataaluma, wazazi, walezi pamoja na wahitimu.
....





No comments:
Post a Comment