Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeipongeza kampuni ya Chusa Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite kwa namna ilivyojitoa na kujenga wodi ya wanawake na watoto kwenye kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kupitia uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility)
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Subira Mgalu amesema makampuni ya madini yanapaswa kuwajibika kwa jamii inayowazunguka (CSR) hivyo kitendo cha Chusa Mining kujenga wodi hiyo Mirerani ni cha kupongezwa.
Mgalu amesema pamoja na hayo pia kitendo cha kampuni hiyo kugawa udongo kwa wanawake na makundi maalum ili wakachekeche na kujipatia chochote kitu ni jambo la kupongezwa.
Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa jamii inayowazunguka ikiwemo kujenga wodi ya wanawake na watoto.
"Kwenye kituo cha afya Mirerani tumejenga jengo la wodi ya kulaza wanawake, watoto na ofisi ya madaktari katika kuunga mkono huduma za jamii kupitia CSR," amesema Mwakipesile.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Chacha Wambura maarufu kama Waja ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Geita mjini amempongeza Chusa kwa kugawa udongo kwa makundi maalum ili nao wajitafutie kipato.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala amesema Chusa Mining LTD na Franone Mining & Gem LTD wamekuwa wakitoa mchanga bila kudai malipo kwa wadau wanaochekecha na kupata fedha za kujikimu.
Afisa Madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Mirerani (RMO) George Kaseza amesema kitendo cha migodi kuwapa udongo wahitaji mbalimbali kinapaswa kuungwa mkono.
"Kwa siku watu 20,000 huingia ndani ya ukuta wakiwemo wamiliki wa migodi, wasimamizi wa migodi, wachimbaji, wanunuzi wenye leseni, wachuuzi na wajasiriamali hivyo mgodi kutoa udongo bila kulipwa ni uungwana mzuri kwani wengine huwa wanauza," amesema Kaseza.
MWISHO

No comments:
Post a Comment