Na Lilian Kasenene, Morogoro
Maipacarusha20@gmail.com
BAADHI ya ndugu waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuchukuliwa vipimo vya vinasaba (DNA) kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao waliofariki katika ajali ya basi la Green Line wamelalamikia kuchelewa kwa majibu ya vipimo hivyo.
Ndugu hao walisema hali inawafanya kutokuwa na uhakika wa lini watakabidhiwa miili ya wapendwa wao kwa ajili ya mazishi.
![]() |
| Raphael Mapambano,ndugu wa marehemu ajali Morogoro |
Miili 17 ya watu waliofariki na kuteketea kwa moto katika ajali hiyo iliyotokea Oktoba 8, mwaka huu, eneo la Mkambarani, mkoani Morogoro, imetambuliwa kwa njia ya vipimo vya DNA, huku miili 16 ikiwa tayari imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 12, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Best Magoma, amesema zoezi la utambuzi wa miili mingine iliyosalia linaendelea kufanywa na Ofisi ya Taifa ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika.
Kuhusu majeruhi wa ajali hiyo, Dk. Magoma alisema wote wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya hali zao kuimarika, huku majeruhi wa mwisho akiruhusiwa leo asubuhi.
Alisema zoezi la utambuzi wa miili linafanyika kisayansi na linahusisha vyombo na mamlaka mbalimbali, hivyo taarifa iliyotolewa si ya mwisho, kwani taarifa ya jumla itatolewa baada ya zoezi hilo kukamilika.
“Hili zoezi la utambuzi linafanywa kisayansi na linashirikisha vyombo na mamlaka mbalimbali, hivyo hii si taarifa ya mwisho, bali tutatoa taarifa ya jumla baada ya kazi hii kukamilika,” amesema Dk. Magoma.
Kwa upande wao, baadhi ya ndugu waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa sampuli za DNA wamesema kuchelewa kwa majibu hayo kumewaacha katika hali ya sintofahamu, huku wakiendelea kusubiri taarifa kuhusu miili ya ndugu zao.
Raphael Mapambano baba wa Marehemu Neema Raphael alisema alifika hospitalini hapo Jumamosi akitokea mkoani Mbeya kwa lengo la kutafuta miili ya watoto wake wawili, mmoja akiwa mtoto wake wa kumzaa na mwingine mtoto wa kaka yake.
Alisema baada ya kufika hospitalini hapo alichukuliwa sampuli za vinasaba, lakini hadi sasa hajapata majibu, huku akilazimika kulala katika maeneo ya hospitali hiyo akisubiri majibu na kukabidhiwa miili ya watoto hao.
“Mabinti zangu hao walikuwa wakitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya baada ya kumaliza field. Mmoja ni binti yangu wa kumzaa, anaitwa Neema Raphael, na binti wa kaka yangu anaitwa Dola Moses,” alisema Mapambano.
Aidha, Mapambano amelalamikia kile alichokiita kutowajibika kwa baadhi ya kampuni za mabasi linapotokea tukio la ajali, akidai kuwa kampuni hizo zimekuwa hazitoi ushirikiano wa kutosha katika masuala ya bima.
Alisema serikali imekuwa haichukui hatua za kutosha dhidi ya kampuni zinazoshindwa kutekeleza wajibu wao wa bima kwa majeruhi na familia zilizofiwa, huku akiiomba serikali kusimamia suala hilo na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.
Naye Athuman Ndosi, baba wa aliyekuwa dereva wa basi hilo la Green Line, amesema amesikitishwa na kile alichodai kuwa ni kutelekezwa na mmiliki wa basi hilo, ambaye alikuwa mwajiri wa marehemu mwanawe, Silaji Athuman.
“Tangu tumefika hapa hakuna mazungumzo yoyote na mmiliki wa basi, wala hajui tunakula wapi au tunalala wapi. Nimekuja na mke wa marehemu na watoto wake, lakini hakuna msaada wowote,” alisema Ndosi.
Katika hali ya kusikitisha, Ndosi alisema familia yao ilikabidhiwa vipande vya mwili wa mwanawe jana baada ya kupatikana kwa majibu ya DNA, na tayari wamekwenda kuvizika katika Makaburi ya Kola, mkoani Morogoro.
Hata hivyo, alisema baadaye walipewa taarifa kuwa huenda wakapata vipande vingine vya mwili wa marehemu kikiwemo kichwa na mkono.
“Kama familia, imebidi tuzike hapa hapa Morogoro, licha ya kwamba tunatokea mkoani Arusha. Hata tukipata vipande vingine, tutakwenda kuvizika kwenye kaburi lilelile,” alisema Ndosi.
Joyce Mwaisangu, mkazi wa Mbeya, alisema amefika hospitalini hapo kutafuta mwili wa binti yake ambaye alikuwa mfanyabiashara, akieleza kuwa anaamini binti yake ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.
Alisema kabla ya safari, binti yake alimweleza kuwa amepanda basi hilo la Green Line na alikuwa amekaa siti namba tano.
Joyce ameiomba serikali kuwasaidia yeye na familia nyingine zilizofiwa kupata usafiri wa kusafirisha mabaki ya miili ya wapendwa wao kwenda katika mikoa wanayotoka kwa ajili ya mazishi.
Alisema janga hilo limezikumba familia kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo ile ya mbali na Morogoro, hivyo gharama za kusafirisha mabaki ya miili ni kubwa na zinahitaji msaada wa serikali.
Mwisho.

.jpg)
No comments:
Post a Comment