WAFUGAJI WATATU WANATUHUMIWA KUMTOROSHA MWANAFUNZI WA SEKONDARI SOKOINE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 30 October 2026

WAFUGAJI WATATU WANATUHUMIWA KUMTOROSHA MWANAFUNZI WA SEKONDARI SOKOINE

 

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, ACP Andrew Kantimbo


 Lilian Kasenene, Morogoro


Maipacarusha20@gmail.com 


WATU watatu wanaofanya shughuli za ufugaji wanatuhumiwa kumtorosha mwanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Sokoine Memorial, iliyopo wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, kisha kumficha katika eneo la wafugaji.


Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, ACP Andrew Kantimbo, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Kandolo Rosingo Kibasisi (56), mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Sokoine, Michael Jackson Shabala (32) na Ngale Hagiro (41), wote wakazi na wafugaji katika eneo hilo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilitokea Oktoba 26, 2026, majira ya saa 3:00 asubuhi katika eneo la Wami Sokoine, kijiji cha Wami Sokoine, Kata ya Dakawa, wilayani Mvomero.


Inaelezwa kuwa mwanafunzi huyo alitoroshwa na kupelekwa katika makazi ya wafugaji, ambako alifichwa kwa muda kabla ya kukutwa na watu hao.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa vitendo vya baadhi ya wafugaji kuwashawishi wanafunzi kuacha shule na kujiunga na shughuli za ufugaji, huku wengine wakidaiwa kutumia nguvu kuwachukua watoto kutoka kwa familia zao.


Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limeonya dhidi ya vitendo hivyo na kutoa wito kwa jamii, hususan wafugaji, kuacha mila na desturi potofu zinazochangia kuwanyima watoto haki ya kupata elimu.


Aidha, limewataka wazazi na walezi kusimamia watoto wao, kuwahimiza kuendelea na masomo na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapobaini viashiria vya vitendo vya kuwatorosha au kuwashawishi wanafunzi kuacha shule.


Polisi imesisitiza umuhimu wa kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanapata fursa ya kutimiza ndoto zao kupitia elimu.


......

No comments: