Wanawake wazidi kutamba uwakilishi bungeni Tanzania - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 5 October 2026

Wanawake wazidi kutamba uwakilishi bungeni Tanzania

 





Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza uwakilishi wa wanawake Bungeni, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika michakato ya maamuzi.


Zungu amesema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati akihutubia Jukwaa la Wabunge Wanawake katika Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (Arusha), akibainisha kuwa wanawake kwa sasa wanawakilisha asilimia 39.5 ya Wabunge Tanzania.


Amesema hatua hiyo ni ya kutia moyo, lakini uwakilishi pekee hautoshi bila kuendelea kuondoa vikwazo vinavyoathiri ushiriki, uongozi na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kisiasa na kibunge.


“Uwakilishi pekee hautoshi. Ni lazima tuendelee kushughulikia vikwazo vinavyoathiri ushiriki, uongozi na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kisiasa na kibunge,” amesema Zungu.


Amesema mabunge jumuishi yanaimarisha demokrasia na kuchangia katika kujenga mifumo ya utawala inayowakilisha na kuitikia mahitaji ya wananchi kwa upana zaidi.


Zungu amesema kaulimbiu ya Mkutano wa 153 wa IPU, “Kuimarisha Utawala Bora na Kuwezesha Jamii kupitia Ushirikishwaji, Imani na Fursa kwa Wote,” inaendana na umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi katika ngazi zote.

No comments: