WATOTO 10 WENYE HYDROCEPHALUS NA SPINA BIFIDA KUPEWA RUFAA YA MATIBABU MUHIMBILI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 28 October 2026

WATOTO 10 WENYE HYDROCEPHALUS NA SPINA BIFIDA KUPEWA RUFAA YA MATIBABU MUHIMBILI

 


 



Na Lilian Kasenene, Morogoro 


Maipacarusha20@gmail.com 


WATOTO 10 kati ya 58 wenye changamoto za kiafya za kichwa kikubwa (Hydrocephalus) na mgongo wazi (Spina Bifida) mkoani Morogoro wanatarajiwa kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.


Aidha hatua hiyo inalenga kuboresha afya zao na kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za kibingwa, zinazochangiwa na gharama za matibabu na usafiri.


Zoezi la utoaji wa huduma hizo limeanza Oktoba 20 mwaka huu katika Zahanati ya Polisi mkoani Morogoro, likihusisha madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI), kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi. 


Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.


Akizungumzia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, Francis Duwe alisema miongoni mwa changamoto hizo ni upatikanaji wa vifaa saidizi na gharama kubwa za matibabu, ambazo familia nyingi zisizo na uwezo wa kifedha hushindwa kumudu. Hali hiyo huwafanya baadhi yao kukosa huduma za afya wanazohitaji.


Kwa upande wake, Dkt. Hamis Shabani, daktari bingwa wa upasuaji kutoka MOI, amesisitiza umuhimu wa kuwafikia watoto wenye Hydrocephalus na Spina Bifida kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa. Amesema hatua hiyo itasaidia kubaini mahitaji yao ya kiafya na kuwaunganisha na huduma stahiki kwa wakati.


Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dk. Christina Guveti, alisema kuna umuhimu wa kuimarisha mikakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii, hususan watoto wenye ulemavu. Ameeleza kuwa juhudi hizo zinalenga kupunguza vikwazo vinavyowakabili na kuhakikisha wanapata matibabu wanayohitaji kwa wakati.

KKamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, alitoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuacha ubaguzi dhidi ya watoto wenye ulemavu.


Aliwahimiza kuwapa watoto hao upendo, ushirikiano na msaada unaohitajika ili waweze kupata huduma za afya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.


Zoezi hilo linatarajiwa kuwawezesha watoto wenye uhitaji wa matibabu zaidi kupata rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huku likilenga kupunguza changamoto za kifedha na usafiri zinazozikabili familia zao katika jitihada za kutafuta huduma za kibingwa.


.....

No comments: