ATC YAIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI KUPITIA KIWANDA CHA UJIFUNZAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 14 November 2026

ATC YAIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI KUPITIA KIWANDA CHA UJIFUNZAJI

 





Na Mwandishi wetu,Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kimeendelea kuimarisha mifumo ya ufundishaji kwa kuanzisha Kiwanda cha Ujifunzaji (Teaching Factory), kinacholenga kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia duniani.


Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi kupata mafunzo yanayochanganya nadharia na vitendo, ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za mazingira halisi ya kazi.


Akizungumzia mpango huo, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Mussa Chacha, ameeleza kuwa mfumo wa Kiwanda cha Ujifunzaji utawapa wanafunzi fursa ya kujifunza huku wakishiriki katika shughuli halisi za uzalishaji.


Profesa Chacha amesema dhana hiyo inalenga kuboresha namna wanafunzi wanavyopata ujuzi, kwa kuwapa nafasi ya kufanya kazi kwa vitendo sambamba na kuendelea na masomo yao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Fredrick Salukele, ameeleza umuhimu wa kuimarisha mafunzo ya ufundi ili yaendane na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia.


Kupitia mfumo huo, wanafunzi wanatarajiwa kujengewa uwezo wa kutumia teknolojia, kubuni bidhaa na kutoa huduma zinazoweza kukidhi mahitaji ya jamii.


Aidha, Kiwanda cha Ujifunzaji kinatarajiwa kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta ya viwanda, hatua itakayosaidia kuziba pengo kati ya elimu inayotolewa vyuoni na ujuzi unaohitajika katika maeneo ya kazi.


Hatua hiyo pia inalenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuanzisha shughuli za uzalishaji, badala ya kutegemea ajira pekee.


Kwa ujumla, mpango huo unaonesha jitihada za Chuo cha Ufundi Arusha katika kuboresha elimu ya ufundi na teknolojia kwa lengo la kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.

No comments: