Chongolo ataka umwagiliaji wa matone kuongeza uzalishaji wa ndizi Rombo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 1 November 2026

Chongolo ataka umwagiliaji wa matone kuongeza uzalishaji wa ndizi Rombo

 

Waziri wa kilimo, Daniel Chongolo akizungumza na wananchi wa soko la Mamsera, wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na teknolojia, Profesa Adolf Mkenda


Mwandishi wetu, Rombo


maipacarusha20@gmail.com 


Rombo. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya mapitio ya kina ya matumizi ya maji ya Mto Ungwasi wilayani Rombo, ili kuyawezesha kutumika kwa mfumo wa umwagiliaji wa matone na kuongeza uzalishaji wa ndizi.


Chongolo amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatawezesha wakulima kutumia maji kidogo, huku wakipata mazao mengi na kuongeza tija katika kilimo cha ndizi.


Chongolo ametoa agizo hilo jana  wakati alipotembelea eneo hilo la mto Ungwasi lenye chanzo kikubwa cha maji katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.


Chongolo amesema iwapo maji ya Mto Ungwasi yataweza kudhibitiwa na kuelekezwa mashambani kwa mfumo wa mserereko, wakulima watapata fursa ya kuyatumia kwa ufanisi zaidi katika shughuli za uzalishaji.


"Nataka Tume ya Umwagiliaji ifanye mapitio makubwa ili Mto Ungwasi uwe na tija kubwa. Kama tunaweza kuyashika maji na kuyaingiza kwenye mashamba kwa mserereko, kutakuwa na tija kubwa na itakuwa rahisi kwa sababu maji yatakwenda kwenye mashamba.


"Umwagiliaji wa matone unaokoa maji, tunatumia maji machache lakini tija yake ni kubwa sana. Tunataka hilo tulifanye ili tupate tija hiyo," amesema Chongolo.


Amesema Serikali pia inataka kuwaunganisha wakulima wa Rombo na mifumo ya usafirishaji na masoko ya kimataifa inayotumiwa na wakulima wa maeneo mengine nchini ambao tayari wameanza kuuza ndizi nje ya nchi.


Akitolea mfano, amesema wapo wakulima wa ndizi Rufiji ambao wameanza kuingiza mazao yao katika masoko ya nje ya nchi, hivyo ni muhimu kujifunza mfumo wanaoutumia ili wakulima wa Rombo nao wanufaike.


"Nataka kupitia hilo tuunganishe mfumo wanaoutumia kusafirisha wale na sisi tuanze kunufaika na mfumo huo huo," amesema



Amesema Serikali inaweza kutumia miundombinu iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)  ili wakulima waweze kuhifadhi bidhaa zao na kuzisafirisha moja kwa moja kwenda katika masoko ya Kimataifa.


Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uharibifu wa mazao baada ya kuvunwa na kuwawezesha wakulima wa ndizi na mazao mengine kufikia masoko ya kimataifa kwa urahisi.


Naye,  Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wakulima wanahitaji kusaidiwa kujenga mfumo wa umwagiliaji wa matone utakaowawezesha kutumia maji ya Mto Ungwasi kwa muda mrefu.


Amesema mfumo huo utasaidia kuhakikisha kila shina la mgomba linapata maji ya kutosha kupitia mrija maalumu unaodondosha maji taratibu.


"Tunaomba Wizara itusaidie tujenge mfumo wa umwagiliaji wa matone ili yale maji ya Ungwasi tuweze kuyatumia kwa muda mrefu. Kila shina la mgomba lipate mrija wa kuweka matone ya maji. Tuvune kisasa, tupate mazao mengi ili tufaidike na soko hili," amesema Profesa Mkenda


Amesema mfumo huo utawasaidia wakulima kubaki na umiliki wa mashamba yao huku wakishirikiana katika kutafuta masoko na kupanga namna bora ya kuuza mazao yao ili kuongeza kipato.


"Unaweza kuwa na shamba lako, mwingine akawa na lake, lakini tukafanya ushirika. Tukahakikisha tunavuna na tunauza kwa pamoja ili kuhakikisha kipato chetu kinaongezeka," amesema Profesa  Mkenda

No comments: