DIWANI NABERERA ALIA NA TEMBO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 2 November 2026

DIWANI NABERERA ALIA NA TEMBO

  

DIWANI wa Kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Marco Munga


Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com 


DIWANI wa Kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Marco Munga ameiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya tembo waliovamia baadhi ya makazi ya kijiji cha Naberera.


Munga ameeleza hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika makao makuu ya Wilaya hiyo mji mdogo wa Orkesumet.


Amesema baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameshikwa na hofu na taharuki kutokana na matukio ya tembo kuvamia makazi na kusababisha mauaji.


"Wiki iliyopita kuna kijana mdogo wa miaka 16 ameuawa na tembo na hivyo kusababisha hofu kwa wakazi wa eneo hilo, tunaomba hatua ichukuliwe ili kudhibiti tembo hao," amesema Munga.


Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Kaleya Melita Mollel ametoa pole kwa wananchi wa eneo hilo na wa maeneo mengine ya Simanjiro waliokumbwa na adha ya tembo.


Mollel amesema Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ashirikiane na TAWA ili kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti wanyama waharibifu.


"Pia, utaratibu wa kulipa waathirika kifuta jasho au kifuta machozi uendelee kufuatiliwa ili wahusika wawe wanalipwa fedha hizo," amesema Mollel.


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amesema wameweka mikakati kwa kushirikiana na TAWA ili kukomesha hali hiyo.


Makota amesema wameweka mikakati ya kupambana na kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya vitongoji, vijiji na nyumba za ibada kwa kuwapa mbinu na zana za kupambana na tembo.


Amesema vituo vya kupambana na wanyama waharibifu vinajengwa na kuanzia kijiji cha Kandasikira na kingine kitajengwa kijiji cha Naberera.


Kwa upande wake, Afisa wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Aloyce Olodonjilalo amesema hivi sasa kuna kikosi cha doria kinachoendelea na msako wa tembo hao.


Olodonjilalo amesema  ndege nyuki moja imeshapatikana kupitia Tawa kwa ajili ya kufukuza na kuhamisha tembo pia askari wameongezwa baada ya kupatiwa mafunzo na wengine kupelekwa chuo cha Sekamaganga Tabora.


MWISHO

No comments: