MKULAZI KULENGA KUZALISHA TANI 50,000 ZA SUKARI MSIMU WA 2028/2029 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 26 November 2026

MKULAZI KULENGA KUZALISHA TANI 50,000 ZA SUKARI MSIMU WA 2028/2029

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro

Maipacarusha20@gmail.com 


Kampuni ya Mkulazi inatarajia kuzalisha tani 50,000 za sukari katika msimu wa 2028/2029, baada ya kukamilisha upandaji wa miwa na uwekaji wa mfumo wa umwagiliaji katika mashamba yenye ukubwa wa hekta 4,156 ifikapo Juni 30, 2027.


Meneja wa Idara ya Kiwanda wa kampuni hiyo, Mhandisi Aron Mwaiganga, amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kampuni kwa Jukwaa la Wahariri.


Amesema kampuni hiyo imeweka mpango mkakati wa kuongeza ufanisi wa uzalishaji kwa kununua na kutumia teknolojia, zana na utaalamu wa kisasa wa kilimo ili kufikia asilimia 100 ya malengo ya uzalishaji.


Ameeleza kuwa kwa sasa jumla ya hekta 3,548 zimepandwa miwa, sawa na asilimia 85 ya lengo la upatikanaji wa miwa kwa ajili ya uzalishaji.


Mwaiganga ameongeza kuwa, mbali na kuendeleza mashamba yake, kampuni hiyo pia inanunua miwa kutoka kwa wakulima wadogo 304 wanaozunguka kiwanda hicho, ambao wamesajiliwa na Bodi ya Sukari Tanzania.


Amesema ili kuhakikisha upatikanaji wa miwa yenye ubora na kuongeza tija, kampuni ya Mkulazi imekuwa iki wakopesha wakulima hao mbegu bora za kisasa, ambapo hadi Novemba mwaka huu imewakopesha mbegu zenye thamani ya shilingi bilioni 1.04.


Aidha, amesema kampuni hiyo imeingia makubaliano na Bodi ya Sukari Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika uanzishwaji wa kitalu cha mbegu bora, hatua itakayowawezesha wakulima wadogo kupata mbegu bora na kuongeza uzalishaji wa miwa.


Mwaiganga alikuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kampuni ya Mkulazi kwa wajumbe wa Jukwaa la Wahariri waliopo mkoani Morogoro kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa Tisa wa jukwaa hilo, unaotarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Dkt. Lameck Mwigulu Mchumba.

....

No comments: