Na Mwandishi wetu, Babati
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege amekabidhi shilingi milioni 16 na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Mkoa wa Manyara.
Naibu Waziri Regina ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, katika fedha hizo ameweka shilingi milioni 10 kwenye akaunti ya ujenzi ya benki ya msikiti huo.
Amemkabidhi fedha taslimu shilingi milioni sita Sheikhe wa Mkoa wa Manyara, Alhaj Muhammad Kadidi na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo.
Akizungumza baada ya kukabidhi fedha hizo na mifuko hiyo ya saruji Naibu Waziri Ndege amesema fedha hizo amezitoa kwa kushirikiana na wadau wake wa maendeleo .
"Tutaendelea kushirikiana pamoja na kuunga mkono ujenzi huu wa msikiti kadiri tutakavyojaliwa na Mungu," amesema Naibu Waziri Regina.
Kwa upande wake, uongozi wa msikiti huo umempa hati ya pongezi Naibu Waziri Regina kwa kutambua mchango mkubwa anaoutoa katika ujenzi wa msikiti huo, unaotegemea kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Sheikhe wa Mkoa wa Manyara Alhaji Muhammad Kadidi na uongozi wa msikiti huo wamemshuku Naibu Waziri Regina na kumuombea dua.
Naibu Waziri Regina ameambatana na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Manyara, Fatuma Tsea ambaye amempongeza Naibu Waziri Regina kwa namna anavyojitoa kwa jamii bila kujali madhehebu ya dini.
MWISHO


No comments:
Post a Comment