RC MAKALLA AFIKA MONDULI KUTATUA MGOGORO WA ARDHI KIJIJI CHA MAKUYUNI ULIODUMU KWA MIAKA 20 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 7 November 2026

RC MAKALLA AFIKA MONDULI KUTATUA MGOGORO WA ARDHI KIJIJI CHA MAKUYUNI ULIODUMU KWA MIAKA 20

 

Kampuni ya Rhino Equipment & Transportation ndiyo mmiliki halali lakini Rc Makalla Asisitiza busara na utu, akipendekeza mwekezaji kuridhia kumega ekari 100 kwaajili ya Kitongoji cha Zaburi chenye usajili na miundombinu ya Msikiti, Kanisa, Maji, Umeme na chekechea_

_Rc Makalla amewaambia wakazi hao eneo lingine la Ekari 100 lenye makazi ya kudumu nje ya Eneo  la Ekari 100 ya miundombinu ya jamii, Mwekezaji kukaa na wavamizi na kukubaliana

_Awataka wananchi kuwa watulivu, kusitisha uvamizi na uendelezaji wa eneo hilo mpaka kukamilika kwa makubaliano



- *_Baada ya makubaliano aitaka Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kupanga maeneo yatakayoachwa na Mwekezaji_*


Na Mwandishi Maalumu. RS Arusha


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, leo Ijumaa, Novemba 6, 2026, ametatua mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Monduli, uliodumu kwa takribani miaka 20 baada ya wananchi kuvamia eneo la mwekezaji la ekari 200 na kufanya shughuli za uzalishaji na kuweka makazi.


Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Zaburi, Mhe. Makalla amebainisha kuwa kampuni ya Rhino Equipment & Transportation ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo, huku Serikali ikipendekeza mwekezaji huyo aridhie kutenga ekari 100 kwa ajili ya kitongoji hicho ambacho tayari kimesajiliwa na kina miundombinu mbalimbali ya kijamii ikiwemo msikiti, kanisa, shule ya awali pamoja na huduma za maji na umeme.


Katika maelekezo yake, Mhe. Makalla ameutaka uongozi wa Rhino Equipment & Transportation kukaa na kuzungumza na wananchi walioingia katika eneo lake lingine lenye ukubwa wa ekari 100 na kuweka makazi na kufanya shughuli mbalimbali ili kwa pamoja waweze kufikia makubaliano yatakayowezesha matumizi sahihi ya ardhi hiyo na kuondoa mgogoro.


Mhe. Makalla kadhalika amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuwa watulivu na kusitisha uvamizi na uendelezaji wa maeneo hayo hadi pale makubaliano yote yatakapokamilika suala ambalo limeungwa mkono na Uongozi wa eneo hilo, huku akiiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo na kuhakikisha kunakuwa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi itakayotengwa na mwekezaji kwa ajili ya wananchi hao.

No comments: