SHABOUT AMPONGEZA WAZIRI MAVUNDE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 5 November 2026

SHABOUT AMPONGEZA WAZIRI MAVUNDE

 


Na Mwandishi wetu, Nzega


maipacarusha20@gmail.com 


MDAU wa maendeleo na mchimbaji maarufu wa madini ya dhahabu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Rashed Shabout amempongeza Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde kwa namna anavyoiongoza Wizara hiyo na kuwajali wachimbaji wazalendo.


Shabout katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema anapenda kutoa pongezi zake za dhati na za kipekee kwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, kwa uongozi wake mahiri, uzalendo na usimamizi thabiti wa sekta ya madini nchini Tanzania.


"Ninakupongeza sana kwa kuhakikisha kuwa sekta ya madini inasimamiwa kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, kanuni na sera za nchi, huku ukisimamia kwa vitendo maslahi ya Taifa na wananchi wake," amesema Shabout.


"Kwa namna ya pekee, napenda kukupongeza kwa juhudi zako za kuimarisha na kulinda nafasi ya wachimbaji wadogo wa madini wazawa. 


Amesema hatua ya Waziri Mavunde kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata leseni za uchimbaji madini ni jambo kubwa, la kihistoria na lenye maana pana kwa maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.


"Huu ni ushahidi wa uongozi unaotambua kuwa rasilimali za madini zinapaswa kuwa fursa kwa Watanzania, si kwa wawekezaji wakubwa pekee, bali pia kwa wachimbaji wadogo ambao wamekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa nchi yetu," ameeleza Shabout.


"Mheshimiwa Waziri, kwa kuwapa wachimbaji wadogo wazawa nafasi, haki na fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini, unajenga msingi wa uwezeshaji wananchi, kuongeza ajira, kukuza mitaji ya wazawa na kuhakikisha kuwa utajiri wa rasilimali zetu unachangia maendeleo ya Taifa," amesema.


Ametoa hongera kwa Waziri Mavunde kwa kusimamia sekta hiyo muhimu kwa vitendo, kwa ujasiri na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.


"Tunaomba uendelee na kasi hii, kwa sababu mafanikio ya sekta ya madini yanapaswa kupimwa pia kwa namna Mtanzania wa kawaida anavyonufaika na rasilimali za nchi yake," amesema Shabout.


Amempongeza na kumpa hongera Waziri Mavunde kwani uongozi wake unaacha alama katika uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wazawa na maendeleo ya sekta ya madini nchini.


"Mungu akujalie hekima, nguvu na afya njema katika kuendelea kulitumikia Taifa letu, hongera sana, Mheshimiwa Waziri!" amesema Shabout.


MWISHO

No comments: