TAKUKURU YATATUA KERO YA MAJI STEShENI YA SGR MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 4 November 2026

TAKUKURU YATATUA KERO YA MAJI STEShENI YA SGR MOROGORO

 


Na Lilian Kasenene, Morogoro


Maipacarusha20@gmail.com 


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imefanikiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Stesheni ya Reli ya Kisasa ya SGR ya Jakaya Kikwete mkoani Morogoro, hatua inayotarajiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 106.08 kwa mwaka zilizokuwa zikitumika kununua na kusafirisha maji kwa magari maalumu.


Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi sita iliyopita, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Casius Kiaro, alisema utatuzi wa changamoto hiyo utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa stesheni hiyo.


"Kwa utatuzi wa changamoto hii ya maji katika stesheni, tunatarajia kuokoa zaidi ya Sh milioni 106.08 kwa mwaka zilizokuwa zikitumika kununua na kusafirisha maji kwa magari maalumu," alisema Kiaro.


Alisema kabla ya hatua hiyo, stesheni hiyo ilikuwa ikitumia Sh milioni 2.21 kwa wiki, sawa na Sh milioni 8.24 kwa mwezi, kwa ajili ya kununua maji yaliyokuwa yakisafirishwa kwa magari maalumu kutokana na kutokuwa na huduma ya maji ya uhakika kwa matumizi ya stesheni na mabehewa ya treni.


Kiaro alisema TAKUKURU, kupitia mpango wake wa ufuatiliaji wa huduma za kijamii, ilibaini changamoto hiyo na kuamua kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupitia mradi wa SGR pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).

Injinia Gidion Chahe meneja kanda namba moja MORUWASA




Kwa upande wake, Meneja wa Kanda Namba Moja wa MORUWASA, Mhandisi Gidion Chahe, alisema kwa sasa matumizi ya maji katika stesheni hiyo ni kati ya lita milioni mbili hadi nne kwa siku, huku huduma ya maji ikitolewa mara mbili kwa wiki.


Alisema ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika zaidi, stesheni hiyo kwa kushirikiana na MORUWASA inaendelea na ujenzi wa matanki makubwa yatakayowezesha kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya siku tatu hadi tano.


Naye Kaimu Meneja wa Stesheni ya Jakaya Kikwete, Salvatory Kimaro, alisema kituo hicho kwa sasa kinahudumia idadi kubwa ya abiria ikilinganishwa na kipindi cha mwanzo, hali inayosababisha ongezeko la mahitaji ya maji.

Kaimu Meneja wa Stesheni ya Jakaya Kikwete, Salvatory Kimaro

"Wakati tunaanza tulikuwa na safari chache na mahitaji ya maji yalikuwa lita 6,000, lakini sasa safari zimeongezeka na abiria wameongezeka. Mahitaji ya maji kwa sasa ni lita 152,000 kwa wiki," alisema Kimaro.


Mwisho..

No comments: